Mgogoro mkubwa umeibuka kwenye mitandao ya kijamii kati ya mchekeshaji maarufu wa Kenya Oga Obinna na sosholaiti maarufu Amber Ray, kufuatia madai tofauti kuhusu ushirikiano wao katika video ya muziki. Wawili hao wameingia kwenye malumbano ya hadharani, kila mmoja akieleza upande wake wa tukio hilo lililotokea hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Oga Obinna, kulikuwa na makubaliano ya awali kati yao ambapo Amber Ray alitakiwa kucheza kama “mrembo wake” kwenye video ya muziki aliyokuwa akiandaa. Obinna anadai kuwa Amber alikubali, alipokea malipo, lakini alipofika kwenye seti ya kurekodi, alichelewa na alikuwa amelewa. Pia alikataa kushiriki kikamilifu kwenye uchezaji na maingiliano yaliyokuwa kwenye script ya video hiyo. Obinna ameenda mbali zaidi kwa kuonyesha “receipts” kwenye Instagram, akisema anachofanya ni kueleza ukweli wake kwa uwazi mbele ya mashabiki wake.
Hata hivyo, Amber Ray hakukaa kimya. Kupitia mitandao ya kijamii, alikanusha vikali madai hayo, akieleza kuwa hakuwa amelipwa pesa yoyote kama ilivyodaiwa. Kulingana naye, alifanya hivyo kama fadhila baada ya Obinna kumpongeza na kumuomba usaidizi wa haraka. Amber anadai kuwa ahadi pekee aliyopata kutoka kwa Obinna ilikuwa ni KSh 40,000 kwa ajili ya mafuta ya gari, lakini fedha hizo hazikuwahi kutumwa. Aidha, alisema hakuwahi kukubaliana kushiriki kwenye uchezaji wa karibu au wa kimapenzi kwenye video hiyo, na aliondoka mara tu alipoona maelekezo hayo hayakuwa sehemu ya makubaliano yao ya awali.
Mume wa Amber Ray, mfanyabiashara Kennedy Rapudo, amejiunga kwenye mjadala huo kwa kumpa mke wake sapoti hadharani. Alimshutumu Obinna kwa kujaribu kumdhalilisha Amber na kuvunja heshima ya mwanamke kwa kutumia hadithi za uwongo.
Mzozo huu umetikisa mitandao ya kijamii huku mashabiki wakigawanyika kati ya kuunga mkono upande wa Obinna au wa Amber Ray. Hashtag kama #ObinnaVsAmber na #AmberReceipts zimeanza kusambaa kwa kasi huku kila upande ukijaribu kudhihirisha kwamba unasimamia ukweli.
Hadi sasa, hakuna suluhisho limepatikana, na hali inaonekana kuzidi kuwa mbaya kadri kila mmoja anavyoendelea kuchapisha ushahidi wake na maelezo mapya. Wengi wanajiuliza kama mzozo huu utaisha hivi karibuni au utaendelea kuwa kiki ya mitandao kwa siku kadhaa zijazo.