MSANII MAARUFU WA BANGO PWANI MANU BAYAZ ASEMA HAAAMINI MASHINDANO YA AWARDS MTANDAONI
By Dayo Radio
Published on 09/06/2025 09:21
Entertainment

 

Msanii mashuhuri wa nyimbo za Bango kutoka ukanda wa Pwani, Manu Bayaz, ameibua mjadala baada ya kueleza kutoridhishwa kwake na mashindano ya tuzo (awards) yanayoandaliwa kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumza kwa hisia, Manu Bayaz amesema kuwa mashindano hayo hayatoi picha halisi ya mchango na ubora wa wasanii kwenye muziki wa Bango, kwani yanategemea zaidi umaarufu wa msanii mtandaoni kuliko kazi anazofanya kwa ground.

> "Unakuta msanii ana mashabiki wengi mtandaoni, anakuwa na usemi mkubwa, basi anapita tu kwenye hizo tuzo. Wakati kuna wasanii wengine wanaofanya kazi bora lakini hawana nguvu ya mitandao, hawapewi nafasi," alisema Manu Bayaz.

Msanii huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kukuza muziki wa Bango Pwani, anasisitiza kuwa kuna haja ya kuangalia njia mbadala ya kuandaa mashindano ya tuzo, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila msanii kwa kuzingatia kazi na mchango wake halisi, si kwa kupigiwa kura mitandaoni pekee.

> "Ningeweza kuunga mkono mashindano kama haya kama yangekuwa yanaangalia performance halisi, siyo followers au likes tu. Hapo ndipo kila msanii angepewa heshima yake," aliongeza.

Kauli ya Manu Bayaz imezua mjadala miongoni mwa mashabiki na wadau wa muziki wa Bango, huku baadhi wakimuunga mkono na wengine wakisema mitandao ni sehemu ya maisha ya sasa ambayo kila msanii anapaswa kuitumia ipasavyo.

Comments
Comment sent successfully!