Wanachama wa Kenya Scouts Association wamepanda jumla ya miti 5,000 ya mikoko kwa wakati mmoja leo katika eneo la mikoko la , eneobunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, katika zoezi lililowezesha Kenya kuweka rekodi mpya ya dunia ya watu wengi zaidi kupanda miti ya mikoko kwa wakati mmoja.
Zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano kati ya Kenya Forest Service (KFS), Kenya Scouts Association (KSA) na M-PESA Foundation, likiwaleta pamoja washiriki 4,196, wakiwemo wanachama wa Scouts, wanajamii na wahifadhi wa mazingira. Kati yao, washiriki 4,124 wamekidhi kikamilifu masharti ya Guinness World Records na kuiwezesha Kenya kuvunja rekodi ya awali iliyohitaji angalau washiriki 3,001 kupanda miti kwa wakati mmoja.
Akizungumza na wanahabari baada ya zoezi hilo, afisa wa huduma ya misitu Kenya (KFS), Dkt. Clement Ng'oriareng, amesema mafanikio hayo yanaonyesha kuwa Kenya imejiimarisha kama kinara wa dunia katika juhudi za kurejesha misitu na kuhifadhi mazingira.

"Tulichoshuhudia leo katika eneo la mikoko la Jomvu si jambo la kawaida. Ninaweza kuthibitisha kuwa kati ya washiriki 4,196, jumla ya 4,124 wamekidhi viwango vya juu vya uratibu na usahihi vinavyohitajika na Guinness World Records. Zaidi ya rekodi hii, Kenya imeonyesha kuwa ni kinara wa dunia katika urejeshaji wa misitu. Kila mche umepandwa kwa kuzingatia misingi ya kisayansi ili kuhakikisha manufaa ya kudumu kwa mazingira na uchumi wa buluu," amesema Dkt. Ng'oriareng.
Kwa upande wake afisa mwandamizi wa uhifadhi wa misitu wa KFS, Boniface Mulwa, amesema mafanikio hayo yamethibitisha uwezo wa Kenya wa kutekeleza shughuli kubwa za uhifadhi wa mazingira kwa kufuata viwango vya kimataifa.

"Chini ya uangalizi wa Guinness World Records, Scouts 4,196 pamoja na maafisa 50 wa KFS wamehakikisha zoezi linafanyika kwa mafanikio makubwa. Washiriki 4,124 wameiwezesha Kenya kuweka rekodi mpya ya dunia huku tukijenga msingi wa kulinda mazingira na kuimarisha maisha ya jamii za pwani," amesema Mulwa.
Mafanikio hayo yanaunga mkono azma ya Serikali ya Kenya ya kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032 na kuongeza kiwango cha uoto wa misitu nchini hadi asilimia 30, huku yakichangia uhifadhi wa mikoko, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uchumi wa bahari.
NA HARRISON KAZUNGU.