MBUNGE WA JOMVU BADI TWALIB ASISITIZA UMUHIMU WA UHIFADHI WA MAZINGIRA WAKATI WA ZOEZI LA KIHISTORIA LA UPANDAJI WA MITI 5,000 YA MIKOKO JOMVU.
By Dayo Radio
Published on 27/07/2026 10:44
News

Mbunge wa Eneobunge la Jomvu, kaunti ya Mombasa, Badi Twalib, ametoa wito wa kutunza mazingira ya bahari kwa wakazi wote akita juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira zinapaswa kupewa kipaumbele na kila mwananchi ili kuhakikisha rasilimali za asili zinabaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza wakati wa zoezi la kihistoria la kupanda miti 5,000 ya mikoko kwa wakati mmoja lililofanyika katika eneo la Jomvu Kuu, Kijiji cha kwa Fara, Eneobunge la Jomvu, kama sehemu ya jaribio la Kenya kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness World Records ya watu wengi zaidi kupanda miti kwa wakati mmoja.

Katika hafla hiyo, Mbunge huyo ameungana na Kenya Scouts Association, M-PESA Foundation, viongozi wa serikali, viongozi wa jamii, mashirika mbalimbali, wanafunzi, vijana, wakazi wa Jomvu pamoja na maelfu ya washiriki kutoka sehemu mbalimbali waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo la kihistoria.

      

"Leo nimepata heshima ya kuungana na Kenya Scouts Association, M-PESA Foundation, wanajamii na wadau wengine katika jaribio la kuvunja Rekodi ya Dunia ya Guinness ya watu wengi zaidi kupanda miti kwa wakati mmoja hapa Jomvu Kuu. Hili siyo tu jaribio la kuvunja rekodi, bali ni hatua muhimu ya kuonesha dhamira yetu ya kurejesha mazingira ya ukanda wa pwani, kulinda rasilimali za asili na kuhakikisha tunawaachia vizazi vijavyo mazingira bora na salama," amesema Badi Twalib.

Mbunge huyo amesema miti ya mikoko ina nafasi muhimu katika kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko wa ardhi, kuhifadhi viumbe wa baharini, kuboresha ubora wa hewa kwa kufyonza hewa ya ukaa pamoja na kusaidia jamii zinazotegemea mazingira ya pwani kwa shughuli zao za kiuchumi kama uvuvi.

Aidha, amesema juhudi za upandaji miti ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri maeneo mengi duniani, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, mashirika binafsi, taasisi za elimu na wananchi ndio njia pekee ya kufanikisha malengo ya uhifadhi wa mazingira.

     

Badi ametoa pongezi kwa Kenya Scouts Association, M-PESA Foundation, washirika wa maendeleo, viongozi wa eneo hilo na maelfu ya washiriki waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo, akisema ushiriki wao umeonyesha kuwa jamii ya Jomvu inaelewa umuhimu wa kulinda mazingira na iko tayari kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

"Nawapongeza kwa dhati kila scout, kila kijana, kila mwanajamii, kila mdau na kila mshiriki aliyetoa muda wake kushiriki katika shughuli hii muhimu. Ushiriki wenu umeonyesha kuwa tukisimama pamoja tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uhifadhi wa mazingira yetu. Tuendelee kupanda miti, kuitunza na kuhamasisha jamii kukumbatia mbinu endelevu za kuhifadhi mazingira ili kuijenga Jomvu na Kaunti ya Mombasa yenye mazingira safi, ya kijani na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za tabianchi," ameongeza Badi Twalib.

Zoezi hilo limewaleta pamoja maelfu ya washiriki kutoka makundi mbalimbali ya kijamii walioungana kupanda miti 5,000 ya mikoko kwa wakati mmoja, likiwa sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kurejesha misitu ya mikoko, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuchangia juhudi za Kenya katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku likilenga kuweka rekodi mpya ya dunia kupitia Guinness World Records.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!