Katibu Mtendaji wa IGAD, Dkt. Workneh Gebeyehu, ameandaa kongamano la tatu la kipekee la wajumbe Maalum na Wawakilishi (3rd Special Envoys/Representatives Forum) jijini Nairobi kwa kushirikiana na waziri wa Mambo ya nje na masuala ya Diaspora wa Kenya, Dkt. Musalia Mudavadi.
Kongamano hilo limewaleta pamoja wajumbe kutoka IGAD, Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa mataifa (UN), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (League of Arab States), Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na makundi ya Quartet, Quintet na washirika wengine wa kimataifa ili kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kutafuta suluhisho la mgogoro unaoendelea nchini Sudan.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Dkt. Workneh Gebeyehu amesema kuwa vita vinavyoendelea nchini Sudan vinaendelea kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya raia, uchumi wa taifa hilo na usalama wa ukanda mzima wa Pembe ya Afrika. Amesema hali hiyo imeongeza idadi ya wakimbizi, kuzorotesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kuongeza changamoto za kiusalama katika nchi jirani.
"Mgogoro unaoendelea nchini Sudan una athari kubwa si kwa Sudan pekee bali pia kwa ukanda mzima. Hali hii inahitaji uratibu wa karibu zaidi kati ya washirika wa kikanda na kimataifa kupitia tathmini ya pamoja ya hali ilivyo, ushirikiano wa dhati na mgawanyo wa wazi wa majukumu ili kuongeza ufanisi wa juhudi za kuleta amani," amesema Dkt. Workneh Gebeyehu.

Aidha, amesisitiza kuwa hakuna taasisi au mshirika mmoja anayeweza kutatua mgogoro huo peke yake, hivyo ushirikiano wa pamoja ni muhimu ili kuhakikisha juhudi zote zinaelekezwa katika mwelekeo mmoja unaolenga kurejesha amani ya kudumu nchini Sudan.
Washiriki wa kongamano hilo wamejadili namna ya kuoanisha mikakati ya taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa ili kuepusha kurudiwa kwa juhudi zinazofanana na badala yake kuongeza ufanisi katika juhudi za upatanishi, misaada ya kibinadamu na ujenzi wa amani.
Kwa pamoja, IGAD, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Ulaya, Quartet, Quintet na washirika wengine wamesisitiza kuwa suluhisho la mgogoro wa Sudan lazima liwe linamilikiwa na kuongozwa na wananchi wa Sudan wenyewe, huku jumuiya ya kimataifa ikitoa msaada unaoheshimu maamuzi ya Wasudan.

"Njia ya Sudan kuelekea amani lazima ibaki kuwa ya Wasudan wenyewe. Wajibu wetu kama washirika ni kuratibu juhudi zetu kwa umoja na kuunga mkono mchakato utakaowezesha kupatikana kwa amani ya kudumu, utulivu na mustakabali bora kwa wananchi wa Sudan," wameeleza washiriki wa mkutano huo.
Hata hivyo kongamano hilo hilo linatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa kikanda na kimataifa, huku likitoa msukumo mpya wa kisiasa na kidiplomasia katika juhudi za kumaliza mgogoro wa Sudan na kurejesha amani na utulivu katika eneo la Pembe ya Afrika.
NA HARRISON KAZUNGU.