Mfanyabiashara na mwanamitindo maarufu, Zari Hassan, amemjibu baba wa watoto wake, msanii Diamond Platnumz, baada ya kudai kuwa anaweza kuwa naye kimapenzi wakati wowote atakapohitaji.
Kupitia mahojiano yake ya hivi karibuni, Diamond alidai kuwa licha ya kuwa na maisha yake binafsi, anaweza kumrudia Zari wakati wowote endapo ataamua kufanya hivyo. Kauli hiyo imezua gumzo mitandaoni, huku wengi wakisubiri majibu ya Zari.
Akijibu madai hayo, Zari Hassan amemshutumu Diamond kwa kile alichokitaja kama "ego isiyo na mipaka" na kusema kuwa ni jambo ambalo linapaswa kumalizwa. "Diamond anasumbuliwa na ego ambayo inastahili kumalizwa," alisema Zari kwa msisitizo.
Zari na Diamond walikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda na kupata watoto wawili kabla ya kuachana. Hata hivyo, wameendelea kuwa wazazi wenza, ingawa mara kwa mara wamekuwa wakirushiana maneno kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Taarifa hii inakuja wakati ambapo Zari ameendelea na maisha yake ya ndoa, huku Diamond pia akiwa na mahusiano mapya katika safari yake ya kimapenzi.