Msemaji wa serikali, Isaac Mwaura, ameendelea kuitetea Serikali ya William Ruto akisema kuwa imepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi wa taifa na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Dkt. Mwaura amesema kuwa licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa, Serikali imefanikiwa kuweka mikakati madhubuti iliyosaidia kuleta nafuu kwa wananchi, hususan katika sekta ya kilimo, upatikanaji wa chakula na ajira kwa vijana.
“Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha uchumi wa taifa. Leo hii tunashuhudia bei ya nafaka ikishuka, uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka na mipango ya kuwawezesha wakulima ikiimarika zaidi,” amesema Dkt. Mwaura.
Ameeleza kuwa hatua ya utoaji wa mbegu na mbolea kwa bei nafuu imeongeza uzalishaji mashambani, hali iliyochangia kupungua kwa gharama za chakula sokoni. Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji, ujenzi wa barabara na miundombinu ya masoko ili kuwawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika kwa mazao yao.
“Tumeamua kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa sababu ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu. Matokeo yake sasa yanaonekana wazi kuwa uzalishaji umeongezeka na bei ya vyakula muhimu imeshuka kwa kiasi kikubwa,” amesisitiza.
Katika suala la ajira kwa vijana, Dkt. Mwaura amesema kuwa Serikali imefungua fursa za ajira ndani na nje ya nchi kupitia mikataba ya ushirikiano wa kimataifa pamoja na programu za kuwawezesha vijana kujiajiri.
“Vijana wetu sasa wanapata nafasi za ajira katika masoko ya kimataifa kupitia mikataba tuliyoingia kama taifa. Hii ni hatua muhimu katika kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza kipato kwa familia nyingi,” ameongeza.
Hata hivyo, amewakosoa viongozi wa upinzani kwa kile alichokitaja kuwa ni siasa zisizo na ushahidi, akisema kuwa baadhi yao wamekuwa wakitoa kauli za kupotosha umma bila kuzingatia takwimu rasmi za serikali.
“Ni rahisi kulaumu bila kutoa suluhisho. Tunawaomba viongozi wa upinzani watumie takwimu na hoja zenye mashiko badala ya kueneza hofu na taharuki kwa wananchi,” amesema.
Kauli hiyo inajiri wakati muungano wa upinzani ukiendelea kuishutumu serikali kwa madai ya kushindwa kutekeleza baadhi ya ahadi zake kwa wananchi, hususan katika masuala ya gharama ya maisha na kodi. Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa mageuzi yanayoendelea yanahitaji muda na ushirikiano wa wadau wote ili kuzaa matokeo endelevu.
Dkt. Mwaura amehitimisha kwa kuwataka wananchi kuwa na subira na kuendelea kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kuijenga nchi kiuchumi na kijamii.
“Mwelekeo ni sahihi na dhamira ipo. Tunaamini kwa mshikamano wa kitaifa, tutaendelea kushuhudia mafanikio makubwa zaidi katika siku zijazo,” amehitimisha.
NA HARRISON KAZUNGU.