Zaidi ya vijana themanini katika eneobunge la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, wamepata fursa ya kushiriki katika mdahalo wa uhamasishaji ulioandaliwa na shirika la Amkeni Community kwa ushirikiano na taasisi za serikali zikiwemo IEBC na idara ya usalama. Mkutano huo ulilenga kuwajengea vijana uelewa mpana kuhusu masuala ya usalama, athari za matumizi ya mihadarati, dhuluma za kingono na kijinsia pamoja na umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia kwa kujisajili kama wapiga kura.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika eneo la Manoni, Wadi ya Mtopanga, OCS wa lituo cha polisi cha Kiembeni, Elvis Juma, amewahimiza vijana kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu mustakabali wao wa kimaisha.
“Vijana msikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa au mtu yeyote kwa maslahi yake binafsi. Mkijiingiza katika uhalifu au matumizi ya mihadarati, mtakuwa mnajiandalia matatizo na kuharibu ndoto zenu wenyewe,” amesema Elvis Juma.

Aidha amesema kuwa mkono wa sheria hautachagua mtu, akisisitiza yeyote atakayepatikana atakabiliwa vilivyo huku akisema ni muhimu kila kijana achague njia sahihi mapema ili ajenge maisha yenye heshima.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa shirikahilo Christin Kabuya, ametangaza uzinduzi wa mradi wa “Maskani Yetu For Peace” unaolenga kuwainua vijana kupitia sanaa kama chombo cha kueneza amani.
“Tumeanzisha mradi wa MASKANI YETU FOR PEACE ili kuwapa vijana jukwaa la kutumia vipaji vyao kuhamasisha amani na mshikamano. Tunaamini vijana si chanzo cha matatizo, bali ni sehemu ya suluhisho,” amesema Kabuya.
Wakati uo huo amesema ni muhimu kubadili mtazamo hasi dhidi ya vijana.
“Kupitia muziki, maigizo na sanaa nyingine, vijana wanaweza kubadilisha taswira inayowaonyesha kama wahalifu na badala yake kuwa mabalozi wa amani na maendeleo katika jamii,” ameongeza.
Kwaupande wake mwakilishi wa IEBC pia wametoa wito kwa vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kujisajili kama wapiga kura mara zoezi litakapofunguliwa.
“Ushiriki wenu katika uchaguzi ni sauti yenu. Msipuuze nafasi ya kuamua mustakabali wa nchi yenu kwa sababu mabadiliko huanza na kura,” amesema mmoja wa maafisa wa IEBC.
Baadhi ya vijana waliohudhuria wameeleza kufurahishwa na mpango huo wakisema umewapa mwanga mpya kuhusu changamoto zinazowakabili.
“Mikutano kama hii inatufungua macho. Tunapata elimu kuhusu madhara ya mihadarati na namna ya kujilinda dhidi ya ushawishi mbaya,” amesema mmoja wa vijana.
Kwa ujumla, mkutano huo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha usalama, kukuza uwajibikaji miongoni mwa vijana na kujenga kizazi kinachotambua wajibu wake katika kudumisha amani na kuchangia maendeleo ya taifa.
NA HARRISON KAZUNGU.