“EPUKENI MAENEO YA MAPIGANO NA CHUKUENI TAHADHARI” DKT. ISAAC MWAURA.
By Dayo Radio
Published on 02/03/2026 14:28
News

Msemaji wa Serikali, Dkt. Isaac Mwaura, amesema kuwa serikali inaendelea kujitolea kuhakikisha usalama wa wakenya wanaoishi au kufanya kazi katika mataifa yanayokumbwa na mashambulizi ya kivita. Amesema serikali kupitia wizara husika na balozi zake katika nchi mbalimbali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama katika maeneo hayo ili kuhakikisha raia wa Kenya wanapata taarifa na msaada unaohitajika kwa wakati.

Akizungumza mapema leo na wanahabari jijini Nairobi, Mwaura amewahimiza wakenya walioko katika maeneo yenye mizozo ya kivita hususan katika ukanda wa Mashariki ya Kati kuchukua tahadhari zaidi na kufuata maelekezo ya mamlaka za usalama katika nchi wanazoishi.

“Tunawahimiza wakenya walioko katika maeneo yanayoshuhudia mapigano kuepuka kabisa maeneo ya hatari, kupunguza safari zisizo za lazima na kuhakikisha wanazingatia hatua zote za usalama kwa manufaa yao wenyewe,” amesema Mwaura.

Msemaji huyo ameeleza kuwa serikali imeweka njia mbalimbali za mawasiliano kupitia balozi za Kenya katika nchi husika ili kuwasaidia wakenya wanaoweza kujikuta katika hali ngumu kutokana na mizozo hiyo huku akitaja kuwa balozi hizo ziko tayari kutoa ushauri, msaada wa dharura na mwongozo kwa yeyote anayehitaji.

“Tunawasihi wakenya wote walioko katika maeneo hayo, wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara, kutumia namba za mawasiliano zilizotolewa na balozi za Kenya ili kupata msaada au kutoa taarifa iwapo watakumbana na changamoto zozote,” ameongeza.

Aidha, Mwaura amesisitiza kuwa serikali ya Kenya itaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha raia wake walioko nje ya nchi wanabaki salama licha ya changamoto za kiusalama zinazoweza kujitokeza katika baadhi ya mataifa.

 

“Serikali ya Kenya ina jukumu la kulinda raia wake popote walipo, na tutaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha wakenya walioko nje ya nchi wanapata ulinzi na msaada unaohitajika wakati wote,” amesema.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!