Uwanja wa burudani usiku wa Tuzo za Trace Awards 2024, lakini kilichovuta hisia zaidi ni kitendo cha msanii Harmonize kuinuka na kuanza kuicheza wimbo Komasava wa Diamond Platnumz wakati wa ‘live performance’ yake. Tukio hilo limezua gumzo kubwa mitandaoni, huku mashabiki wakitofautiana kuhusu tafsiri ya kitendo hicho.
Kwa muda mrefu, mashabiki wa Diamond na Harmonize wamekuwa wakibishana kuhusu nani mkali zaidi kwenye muziki wa Bongo Fleva, hasa baada ya Harmonize kujiondoa WCB Wasafi na kuanzisha lebo yake mwenyewe, Konde Gang. Hali hii imekuwa ikichochea ushindani mkali kati ya wawili hao, huku kila upande ukijitahidi kumtetea msanii wao kama bora zaidi.
Baada ya tukio hilo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya mashabiki wamedai kuwa Harmonize alifanya hivyo kama ishara ya heshima na kuthamini muziki mzuri bila kinyongo. Wengine, hasa wale wanaomuunga mkono Diamond, wanadai kuwa hilo ni ishara ya kukubali ubora wa Simba kwenye muziki wa Afrika.
Hata hivyo, kuna kundi la mashabiki wa Harmonize wanaosema kuwa kitendo hicho hakimaanishi lolote zaidi ya kufurahia muziki, huku wengine wakichukulia kama njia ya kupunguza mvutano kati yao na kuonyesha umoja kwenye tasnia ya muziki wa Tanzania.
Kwa vyovyote vile, tukio hili limeongeza moto kwenye mjadala wa nani mkali zaidi kati ya Diamond na Harmonize. Je, hili linatoa ishara ya maridhiano kati yao au ni mwendelezo wa ushindani wa kisanii? Mashabiki wanabaki na maoni tofauti, lakini jambo moja liko wazi—Bongo Fleva inazidi kung’ara kimataifa!