Shirika la Dream Achievers Youth Organisation (DAYO) kwa ushirikiano na TechnoServe kupitia mradi wa Blue Bizz limezindua rasmi mradi wa Mwashi wa muhogo katika kaunti ya Kilifi, hatua inayolenga kuimarisha kilimo cha muhogo, kuongeza ajira na kuchangia usalama wa chakula katika eneo linalokabiliwa na changamoto ya ukame.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mratibu wa miradi katika shirika hilo Enos Opiyo amesema mradi huo umebuniwa kufunguanjia itakayosaidia uzalishaji, ukuaji na hata upatikanaji wa masoko ya uhakika.
Aidha amesema wakulima watawezeshwa kwa mbegu bora, mafunzo ya kilimo cha kisasa na maarifa ya uongezaji thamani ili waweze kupata faida zaidi.

“Tunawapa vijana ujuzi, teknolojia na soko ili muhogo usiwe tena zao la kujikimu tu bali uwe biashara rasmi. Tunataka kuona vijana wanajiajiri kupitia kilimo na wanajitegemea kiuchumi,” amesema Opiyo.
Hata hivyo ameongeza kuwa vikundi vya vijana na wanawake vitapewa kipaumbele kwani wao ndio wanaathirika zaidi na ukosefu wa ajira katika maeneo ya pwani.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa kilimo katika kauntika hiyo Safari Ziro amewahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo akisema muhogo una soko linalokua kwa kasi katika vyakula, lishe na viwanda vidogo vidogo huku akitaja kuwa serikali ya kaunti itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora.
“Kilifi ina mazingira mazuri kwa muhogo. Tukitumia mbinu bora za kilimo na ushirikiano wa wadau, wakulima wataongeza uzalishaji mara kadhaa na kipato kitaongezeka,” amesema Ziro.
Wakati uo huo, waziri wa jinsia, Utamaduni, Masuala ya vijana, michezo na huduma za Jamii Ruth D. Masha amepongeza uzinduzi wa mradi huo akisema unakuja wakati muafaka huku maeneo mengi ya kaunti yakishuhudia uhaba wa mvua.
“Muhogo ni zao linaloweza kuokoa familia nyingi wakati wa ukame. Ni chakula, ni biashara na ni ulinzi wa maisha ya wananchi wetu,” amesema Dama.
Kwa upande wa ukuzaji wa uchumi Bi. Masha amesema kuwa ndio njia bora ya itakayotumika katika kupunguza changamoto za kijamii.

“Kijana akipata kipato hatatafuta njia mbadala zisizo salama za kujikimu. Miradi kama hii inaleta heshima, kipato na matumaini kwa jamii,” ameongeza.
Dama pia ametoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mafunzo na kuunda vikundi ili kunufaika kikamilifu.
“Serikali ya kaunti iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha hakuna kijana anayebaki nyuma. Fursa zipo kinachohitajika ni kujitokeza na kuzitumia,” amesisitiza.
Mradi wa Mwashi wa muhogo unatarajiwa kuwafikia wakaazi wa Chonyi, Chasimba, Matsangoni, Malanga na Rabai ambapo wakulima wadogo wadogo, vijana na wanawake watanufaika kupitia mafunzo, uunganishaji wa masoko na shughuli za uongezaji thamani.
Kupitia mpango huo, wadau wanatarajia kuongeza uzalishaji wa muhogo, kupunguza uhaba wa chakula, kuchochea uchumi wa jamii na kuifanya Kilifi kuwa kitovu cha uzalishaji wa zao hilo katika ukanda wa pwani.
NA HARRISON KAZUNGU.