Aliyekuwa msemaji wa Serikali, Dkt. Isaac Mwaura, amehitimisha rasmi kipindi chake cha kuhudumu baada ya miaka miwili na miezi kumi, huku akizipongeza wizara, idara na mashirika ya umma yaliyofanya vizuri katika mawasiliano na wananchi wakati wa uongozi wake.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika katika jumba la Harambee Annex jijini Nairobi, amesema kipindi chake kimejikita katika kuimarisha mawasiliano ya serikali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu sera, mipango na miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini.
"Mawasiliano bora ni nguzo muhimu ya utawala, kwani husaidia kujenga imani ya wananchi, kueleza sera za serikali na kuonyesha matokeo ya programu za maendeleo," amesema Dkt. Mwaura.

Hata hivyo amesema ushirikiano alioupata kutoka kwa wizara, idara na mashirika mbalimbali ya umma umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utoaji wa taarifa kwa wananchi, hali ambayo imeimarisha uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Katika tathmini yake ya mawasiliano ya umma, ameipa wizara ya hazina ya kitaifa nafasi ya kwanza kwa uwezo wake wa kuwasilisha masuala ya uchumi kwa lugha rahisi na inayoeleweka na wananchi. Aidha, amemsifia waziri wa hazina John Mbadi kwa juhudi zake za kufafanua sera na hatua mbalimbali za kiuchumi zinazochukuliwa na serikali.

"Wizara ya hazina ya kitaifa imeonyesha mfano mzuri wa namna taasisi za umma zinavyoweza kuwasiliana kwa ufanisi na wananchi kwa kueleza masuala magumu kwa lugha rahisi," amesema Dkt. Mwaura.
Wakati uo huo amteja kuwa wizara ya afya imeshika nafasi ya pili kutokana na juhudi zake za kuwafahamisha wananchi kuhusu huduma na programu mbalimbali za afya, huku wizara ya kilimo ikishika nafasi ya tatu kwa mawasiliano yake kuhusu sekta ya kilimo na usalama wa chakula.
Kwa upande wa idara za serikali, amesema Idara ya usalama wa ndani imeongoza kwa utoaji wa taarifa kwa wakati na usimamizi mzuri wa mawasiliano ya umma. Idara za nyumba na maendeleo ya miji, afya ya umma pamoja na masuala ya wakenya wanaoishi nje ya nchi pia zimetajwa kufanya vizuri katika kuwafikia wananchi kupitia mawasiliano ya mara kwa mara.
Katika mashirika ya serikali, mamlaka ya kitaifa ya barabara kuu (KeNHA) imetajwa kuwa bora zaidi kutokana na namna ilivyokuwa ikitoa taarifa kuhusu miradi ya miundombinu na hali ya barabara. Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) imefuata katika nafasi ya pili kwa juhudi zake za kuwafahamisha wananchi kuhusu shughuli za bandari na biashara ya kimataifa.
Aidha, tume ya kitaifa ya jinsia na jsawa (NGEC) imetambuliwa kuwa bora zaidi miongoni mwa tume za kikatiba na taasisi huru kwa juhudi zake za kuelimisha umma kuhusu masuala ya usawa, haki na ujumuishaji.
Dkt. Mwaura amesema mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu kwa taasisi nyingine za umma kuendelea kuimarisha mawasiliano yao ili wananchi waendelee kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu shughuli za serikali.
"Ni wajibu wetu kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati, huku tukikabiliana na taarifa potofu zinazoweza kupotosha umma. Mawasiliano ya serikali yanapaswa kueleza sera kwa wakati, kuonyesha matokeo ya programu za maendeleo na kujenga imani ya wananchi kwa serikali," amesema Dkt. Mwaura.
Ameongeza kuwa mawasiliano ya serikali yanapaswa kuendelea kuzingatia uwazi, ukweli na uwajibikaji ili kuimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi, huku akitoa wito kwa taasisi zote za umma kuendelea kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano kuhakikisha kila mwananchi anapata taarifa muhimu kwa wakati.
NA HARRISON KAZUNGU.