ALI MENZA MBOGO AAPA KUOKOA VIJANA WA KISAUNI KUPITIA ELIMU, AONYA WANASIASA WA VURUGU.
By Dayo Radio
Published on 06/12/2025 21:03
News

Mwenyekiti wa mradi wa Lamu Port South Sudan Ethiopia Transport Corridor (LAPSSET), Ali Menza Mbogo, ameonyesha masikitiko makubwa kufuatia ongezeko la vijana wanaoingia katika uhalifu katika eneobunge la Kisauni, akisema endapo hatua za dharura hazitachukuliwa, kizazi kijacho kitaendelea kuangamia.

Akizungumza katika mkutano wa umasisho wa kina mama eneo la Mtopanga, Mbogo amesema jamii lazima ishikane kuhakikisha vijana wanarudi shuleni na kupewa nafasi ya kuanza upya maisha yao. 

“Vijana wetu wanapotea kwa sababu ya kukosa nafasi na mazingira sahihi ya kujijenga. Tukiwekeza zaidi katika elimu yao, tutapunguza matumizi ya mihadarati, tutapunguza uhalifu, na tutawapa mwelekeo mpya wa matumaini,” amesema Mbogo.

Aidha amesema azma yake ni kuhakikisha hakuna mtoto anayesitisha masomo kwa sababu ya ukosefu wa karo akitaja endapo atapata nafasi ya kuingia malamlakani ataweza kuleta elemu bila malipo huku akiahidi kuwalipia karo watoto kutoka familia zenye changamoto, akisema hatua hiyo itakuwa nguzo muhimu ya kukomesha uhalifu wa vijana.

“Kama watoto wetu watasalia shuleni na kumaliza masomo, tutavunja mzunguko wa umaskini na uhalifu. Hapo ndipo jamii itaanza kuona mwanga mpya,” ameongeza.

Wakati uo huo, amewataja kina mama kuwa wenye mchango mkubwa kwenye safari yake ya kisiasa, akisema wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kutetea maendeleo ya familia na ustawi wa jamii huku akitaja akipewa nafasi ya uongozi atawekeza zaidi ili kuwainua zaidi kimaisha.

“Kina mama wamekuwa nguzo yangu. Wamenipa ujasiri wa kusimama imara na kupigania mustakabali bora wa Kisauni. Nataka kuona maisha yao na ya familia zao yakibadilika kwa njia inayopendeza,” amesema.

Hatavyoamewaonya baadhi ya viongozi wa kisiasa wanawatumia vijana vibaya na kuzua vurugu wakati wa siasa na kuwataka wanasiasa kuuza sera zao kwa amani.

“Siasa sio uwanja wa vita. Kila mtu auze sera zake kwa amani bila kuwachochea vijana kuingia mitaani kufanya vurugu. Vijana wana uwezo mkubwa, tusije tukawaharibia maisha kwa tamaa za kisiasa,” amesema kwa msisitizo.

Amehitimisha kwa kusema kuwa ataendelea kushirikiana na mashirika ya kijamii, viongozi wa dini, walimu na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha vijana wa Kisauni wanapata fursa za kusoma, kujiendeleza na kuondokana na mtego wa dawa za kulevya. 

“Kazi yangu ni kuhakikisha hakuna kijana anapotea. Tutawasimamisha, tutawainua, na tutaibadilisha Kisauni kuwa kitovu cha maendeleo na amani,” amesema.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!