UTABIRI WA HALI YA HEWA WIKI HII
By Dayo Radio
Published on 23/02/2026 11:00
News

Wakaazi wa Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kuchukua tahadhari za hali ya juu kufuatia uwezekano wa kutokea kwa mafuriko ya ghafla katika maeneo mbalimbali, hasa yale ya chini na yenye mabomba hafifu ya kupitisha maji.

Kwa mujibu wa tahadhari za hali ya hewa, mafuriko yanaweza kujitokeza kwa haraka hata baada ya mvua kunyesha kwa muda mfupi.

 Aidha, maji ya mafuriko yanaweza kuonekana katika maeneo ambayo hayajapokea mvua nyingi, hususan maeneo ya tambarare yanayopokea maji yanayotiririka kutoka sehemu za juu.

Wakaazi wameshauriwa kuepuka kuendesha vyombo vya usafiri au kutembea kwenye maji yanayotiririka, pamoja na kutovuka barabara, madaraja au maeneo ya wazi yaliyojaa maji. 

Kwa wakaazi wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa mara kwa mara na mafuriko wanapaswa kuchukua tahadhari mapema ili kulinda maisha na mali zao. 

Hata hivyo wavuvi na wale wanaojihusisha na shughuli za baharini wamehimizwa kufuatilia kwa karibu taarifa rasmi za hali ya hewa ili kuepuka hatari zinazoweza kujitokeza.

Comments
Comment sent successfully!