SERIKALI YATOA MAONO NA MUELEKEO SERIKALI KUHUSU UJUMUISHAJI WA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA MAADHIMISHO YA IDPD 2025.
By Dayo Radio
Published on 04/12/2025 12:09
News

Msemaji wa Serikali, (Dkt.) Isaac Mwaura, ameweka wazi hatua dhabiti zinazotekelezwa na serikali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza hapo jana Jumatano, Desemba 3, 2025, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu (IDPD 2025), amesema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, ni “Fostering Disability-Inclusive Societies for Advancing Social Progress,” akitaja ni mwanga unaowakumbusha wakenya wote kuhusu wajibu wa kitaifa wa kujenga jamii jumuishi inayotambua uwezo wa kila mmoja.

 

“Kaulimbiu ya mwaka huu inatukumbusha kuwa kila mkenya anahesabika na lazima awe na nafasi sawa ya kuchangia maendeleo ya taifa bila ubaguzi. Huu ndio msingi wa Katiba yetu na dira ya taifa.”

Sheria ya watu wenye ulemavu ya 2025 imetoa msingi imara wa kuunganisha sheria za ndani na mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu (UNCRPD), ambao Kenya imejitolea kuutekeleza kwa dhati.

Hata hivyo ameongeza kuwa serikali kupitia ajenda ya mabadiliko ya uchumi (BETA) inaendelea kuimarisha usawa wa upatikanaji wa huduma za kijamii na zile za kiuchumi.

Kwa mujibu wake, sera hizi zinahakikisha watu wenye ulemavu hawakabilii vikwazo vinavyowazuia kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali.

“Tumeweka ujumuishaji kama ajenda kwaku hakuna sekta inayoweza kusonga mbele bila kutambua mchango wa watu wenye ulemavu humu nchini. Serikali hii imejizatiti kuhakikisha hawachwi nyuma katika upatikanaji wa rasilimali, huduma, fursa na ulinzi wa kijamii.”

Katika upande wa ustawi wa jamii, Dkt. Mwaura amesema kuwa mpango wa inua jamii umekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha maisha ya watu wenye ulemavu wa kiwango kikubwa.

“Kupitia inua jamii, idadi ya kuwafikia walemavu imeongezeka zaidi. Hii inaonyesha dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa familia zinazohitaji zaidi ndizo zinazofikiwa kwanza.” 

Vile vile ametaja kuwa serikali imepanua zaidi fursa za kiuchumi kwa kuimarisha biashara ndogo, za kati na zile za juu zaidi kupitia miradi kama hustler fund na programu za kukuza biashara huku watu wenye ulemavu wakiwa wamepata fursa zaidi za kujitegemea kiuchumi.

Amefafanua zaidi kuhusu mageuzi ya mpango wa NYOTA kwa kusema kuwa kama serikali wameondoa sheria ambazo zinazoonekana kuwa kali miongoni mwa walengwa 

“Tumeongeza umri wa vijana wenye ulemavu wanaostahili usaidizi wa NYOTA hadi miaka 35 ili kuondoa pengo la vizazi na kutoa nafasi sawa kwao. Hatuwezi kuwa na usawa wa kiuchumi bila kuwapa vijana wenye ulemavu mazingira bora ya kujijenga.” Amebainisha kuwa zaidi ya vijana 820,000 tayari wameandikishwa na kwamba hatua hii imeleta matumaini mapya kwa kizazi cha vijana wenye ulemavu nchini.

Katika utoaji wa huduma za kijamii na utetezi wa haki, Dkt. Mwaura amesema serikali imekamilisha Sera ya kitaifa ya watu wenye ulemavu ya 2024 na kuimarisha kamati ya ushirikiano wa mamlaka mbalimbali huku akieeleza kuwa mfumo wa Community Based Inclusive Development (CBID) unaoendelezwa na idara ya uwezeshaji na ukuzaji ujuzi kwa watu wenye ulemavu unatoa huduma jumuishi moja kwa moja katika jamii.

“Tunajenga mfumo unaohakikisha huduma zinamfikia mtu mwenye ulemavu mahali anapoishi, si kumweka katika taasisi za kufungiwa. Ni lazima tuondoe vizuizi vya kimazingira ili kila mtu awe huru kushiriki katika maisha ya jamii.”

Amesema pia kuwa vyama vya kisiasa, mashirika ya kijamii na asasi za kiraia vinaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali katika kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye mchakato wa uchaguzi na uongozi.

“Demokrasia haiwezi kuwa kamilifu bila uwakilishi wa kweli wa watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi. Tunahimiza taasisi zote kuendeleza juhudi hizi.” 

Mwaura aidha amesema hatua za kuongeza viongozi wenye ulemavu katika vyombo mbalimbali vya kisiasa ni dalili ya taifa linalojenga mfumo wa uwakilishi unaojali sauti za wote.

Akitaja zaidi kuhusu utekelezaji wa vigezo vya Kenya Kwanza, Dkt. Mwaura amesema serikali imeboresha pakubwa upatikanaji wa huduma za afya zinazojali mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kuongeza vifaa saidizi, kuimarisha huduma za msingi za afya na kueneza huduma za ukarabati katika jamii. 

Ameeleza kuwa huduma za afya lazima zikwe katika hali ambayo watu wenye ulemavu wanaweza kuzipata kwa urahisi ili kupunguza vikwazo vinavyowakabili wanapotafuta matibabu.

Katika elimu, Dkt. Mwaura amesema serikali imeimarisha rasilimali, vifaa, na miundombinu katika shule zinazohudumia wanafunzi wenye ulemavu wa kuona, kama shule ya msingi ya wasioona Thika na shule ya upili ya wasioona Thika.

“Tumeimarisha vifaa vya braille, tumepanua miundombinu na tumeongeza walimu mahiri. Mwaka jana, kupitia juhudi zangu na idhini ya Mheshimiwa Rais, Thika High School for the Blind ilitengewa shilingi milioni 20 ili kuharakisha maboresho yao.”

Akimulika ujumbe wake wa mwisho katika hotuba yake, Dkt. Mwaura ametoa wito kwa wadau wote kuungana ili kujenga taifa jumuishi.

“Hakuna taifa linaloweza kusonga mbele likiwaacha raia wake nyuma. Ujumuishaji wa watu wenye ulemavu ni jukumu letu sote, na ndio msingi wa maendeleo ya kweli.”

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!