Mkurugenzi wa mipango katika wizara ya uchumi samawati Samuel Mukindia, ametoa wito kwa vijana kote nchini kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya bahari kama njia ya kujikomboa kiuchumi na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira unaowakumba.
Akizungumza na wanahabari katika kongamano la malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) linaloendelea mjini Mombasa, Mukindia amesema sekta ya uchumi samawati uko na nafasi zinazoweza kuwanufaisha vijana endapo watazimia ipasavyo
“Sekta ya bahari imejaa fursa nyingi ambazo vijana wakizitumia kikamilifu zinaweza kubadilisha maisha yao. Ni wakati wa vijana wetu kujitosa katika kazi za baharini ili kuepuka changamoto ya ukosefu wa ajira.” Amesema hayo wakati akisisitiza kuwa sekta hiyo bado haijatumika kikamilifu na vijana wana nafasi kubwa ya kufaidika nayo.
Aidha amesema kuwa serikali kupitia wizara ya uchumi samawati imeendelea kupanua maeneo ya mafunzo ya ujuzi, ukarabati wa miundombinu na kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki ipasavyo katika shughuli za baharini.
Mkurugenzi hiyo aidha ametaja kuwa uvuvi wa kisasa, ufugaji wa samaki, usimamizi wa rasilimali za pwani, utafiti wa bahari, teknolojia za baharini, uchakataji wa mazao ya bahari, biashara ya majini na usafirishaji wa baharini kuwa ndiyo yanayobeba fursa kubwa ambazo vijana wanapaswa kuzielekeza nguvu.
Mukindia amesisitiza kuwa uchumi wa samawati ni miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo endelevu nchini, na amesema kuwa sekta hii inaweza kuongeza ajira, kukuza uchumi wa maeneo ya pwani na kuinua maisha ya vijana ikiwa itapewa kipaumbele huku akieleza kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa kuanzisha programu zinazolenga kuongeza ujuzi wa vijana, kuwajengea uwezo wa kubuni miradi na kuwaunganisha na mitaji ili waweze kuanzisha biashara zinazohusiana na bahari.
Aidha, amesema kuwa wizara inatekeleza mikakati mahsusi ya kuongeza usalama na uendelevu katika matumizi ya rasilimali za baharini ili kuhakikisha shughuli za vijana zinakuwa rafiki kwa mazingira na zinaendana na malengo ya SDGs. Ametoa mfano wa juhudi za kupambana na uvuvi haramu, kuimarisha uhifadhi wa mikoko, na kukuza mbinu za ufugaji endelevu wa samaki.
“Kizazi cha sasa kina nafasi ya kujenga mustakabali wake kupitia fursa zilizopo katika uchumi wa uchumi samawati.Tusipoteze nafasi hii, bali tujitokeze kwa ujasiri na kuonesha ubunifu."
Amesema kuwa vijana wamekuwa mstari wa mbele katika ubunifu na wanahitaji tu kupewa mwongozo sahihi ili kugeuza uwezo wao kuwa fursa halisi za kiuchumi.
Kwa ujumla, ujumbe wake katika kongamano hilo umeweka wazi kuwa vijana wakiamua kuchangamkia rasilimali za bahari na kutumia elimu na teknolojia kama nyenzo kuu, wanaweza kukuza maisha yao, kuchangia ukuaji wa uchumi wa Kenya na kuharakisha utekelezaji wa SDGs kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
NA HARRISON KAZUNGU.