KENYA YAAPA KUHARAKISHA UTEKELEZAJI WA SDGs IFIKAPO 2030 – KONGAMANO LA TAIFA LAZINDULIWA MOMBASA.
By Dayo Radio
Published on 26/11/2025 20:59
News

Serikali imeonyesha dhamira thabiti ya kuharakisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030, wakati wa uzinduzi wa kongamano la kitaifa la SDGs la mwaka 2025, linaloendelea mjini Mombasa.

Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau kutoka ngazi za kitaifa, kaunti, mashirika ya umoja wa mataifa, sekta binafsi, asasi za kiraia, vijana, watafiti na jamii kwa ujumla ili kujadiliana hatua za kufanikisha malengo ya maendeleo nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, katibu mkuu katika idara ya mipango ya uchumi, Bonface Makokha, ameeleza kuwa kongamano hilo linafanyika katika kipindi ambacho dunia nzima inakabiliwa na changamoto kubwa ya kasi ndogo ya utekelezaji wa SDGs. 

Katibu huyo aidha amebainisha kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya SDGs ya umoja wa mataifa ya mwaka 2025, ni asilimia 35 pekee ya malengo ya kimataifa yanayoonekana kuwa katika mkondo ufaao, huku asilimia 65 ya malengo hayo.

 

Hata hivyo, Kenya imeendelea kuonyesha uongozi na mwelekeo unaotia matumaini kupitia hatua chanya za maendeleo katika sekta mbalimbali.

 

Makokha aidha ameeleza kuwa kwa mujibu wa tathmini ya kitaifa, Kenya imepiga hatua katika takribani asilimia 61 hatua aliyoitaja kuwa ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati unaoongozwa na serikali kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo na jamii. 

 

Ameongeza kuwa juhudi hizi zinaendana moja kwa moja na ajenda ya Bottom-Up Economic Transformation (BETA), ambayo imeweka kipaumbele kwa sekta zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kama kilimo, afya, elimu na ujasiriamali.

 

Akitoa mifano ya mafanikio yaliyopatikana, Makokha ameeleza kuwa zaidi ya wakulima milioni sita wamenufaika na upatikanaji wa mbolea kwa bei nafuu pamoja na huduma za ugani, hatua iliyoongeza tija ya uzalishaji. Aidha, serikali imeimarisha huduma za afya kupitia usajili wa wanachama 25.8 milioni katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na kuajiri watoaji habari za afya ya jamii 100,000 walioko mashinani ili kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu. 

 

Katika upande wa makazi, amesema mradi wa nyumba za bei nafuu umezalisha zaidi ya ajira 330,000 na kuendeleza miji salama na yenye miundombinu ya kisasa.

 

Hata hivyo ametaja sekta ya uchumi kuwa zaidi ya KSh 74 bilioni zimefikishwa kwa wananchi kupitia hustler fund, hatua ambayo imewezesha mamilioni ya wanabiashara wadogo kupata mitaji ambayo awali haikuwa rahisi kupatikana.

 

Vilevile, amesema kupitia NYOTA Programme, vijana 70 kutoka kila wadi humu nchini wanapata mtaji na mafunzo ya biashara, hatua inayolenga kuimarisha uchumi unaoongozwa na vijana.

 

Makokha amesisitiza umuhimu wa takwimu katika kuharakisha maendeleo.

 

“Takwimu za uhakika ndizo zinazoamua kasi ya maendeleo. Hatuwezi kupima athari, kupanga kikamilifu au kuwafikia walioachwa nyuma bila mfumo imara wa ukusanyaji na uchambuzi wa data.” amesema.

 

Amesema hayo huku akitoa wito kwa wadau wote kuwekeza zaidi katika ujenzi wa mifumo ya kisasa ya takwimu.

 

Katika kuimarisha mfumo huo, Makokha ameeleza kuwa Kenya sasa inaripoti vmatumani yake na kuongezeja kwa mavuno hadi 171 vya SDGs kupitia ushirikiano wa karibu kati ya KNBS, wizara mbalimbali na Serikali za kaunti. Kupitia juhudi hizo, ametangaza kuwa Kenya imepata nafasi ya kuwa mwenyeji wa Global Data Festival 2026, tukio kubwa la kimataifa litakaloiweka nchi katika ramani ya ubunifu wa takwimu na matumizi ya teknolojia katika maendeleo.

 

Kuhusu umuhimu wa ubunifu, teknolojia na ushirikiano, Katibu huyo amenukuliwa akisisitiza kuwa taifa lazima liekeze zaidi kuhusu suala la ubunifu.

 

“Safari ya kufikia SDGs inahitaji ubunifu, ushirikiano wa dhati, na hatua za ujasiri.” amesema Makhoha.

 

Ametoa kauli hiyo akiwataka wadau kujitokeza na suluhu mpya zitakazoharakisha utekelezaji wa malengo hayo kwa manufaa ya wananchi.

 

Makokha ameongeza kuwa kaulimbiu ya kongamano la mwaka huu “Race to 2030 Leveraging Strategic Partnerships, Collaboration and Innovative Financing” inaendana na haja ya nchi kuunganisha nguvu, kubuni mbinu mpya za ufadhili na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi muhimu katika kipindi kifupi kilichosalia kabla ya mwaka 2030. Amewapongeza wadau mbalimbali kwa mchango wao, hususan sekta binafsi, ambayo ameitaja kuwa mhimili muhimu katika ubunifu na uwekezaji wa kifedha.

 

Kongamano hilo la siku tatu linatarajiwa kutoa mapendekezo thabiti, kuimarisha ushirikiano kati ya wadau na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto kama ufadhili mdogo, pengo la takwimu, mabadiliko ya tabia nchi na ukosefu wa usawa wa kiuchumi na kijamii huku washindi wa tuzo za SDGs pia wanatarajiwa kupewa heshima kama namna ya kutambua michango mbalimbali inayochochea maendeleo katika jamii.

 

Kwa kukamilisha hotuba yake, Makokha amewahimiza wadau kutumia majadiliano ya kongamano hili kama fursa ya kuibua mawazo, kuonyesha ubunifu, na kubuni ushirikiano utakaopeleka taifa mbele.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!