Ulimwengu umeadhimisha uzinduzi wa Siku 16 za uhamasishaji dhidi ya ukatili wa Kijinsia mapema leo katika Kaunti ya Mombasa, hafla iliyoleta pamoja wadau mbalimbali wa kupigania haki, mashirika ya kijamii, vijana na watetezi wa jinsia kutoka maeneo mbalimbali ukanda wa pwani. Kauli mbiu ya mwaka huu imeweka msisitizo mkubwa katika kupambana na ongezeko la dhulma za kijinsia katika majukwaa ya kidijitali, suala ambalo linazidi kutishia usalama na ustawi wa watumiaji wa mtandao, hususan wanawake na wasichana.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Janet Molo kutoka shirika la Pwani GBV Network amesema kuwa dhulma za kijinsia mtandaoni zimechangia pakubwa kuongezeka kwa matatizo ya kisaikolojia, unyanyapaa na hata kuathiri mustakabali wa vijana.

“Tumeona visa vya wasichana kujifungia ndani, kusitisha masomo, na wengine hata kuhamia maeneo mengine kutokana na aibu inayotokana na kusambazwa kwa picha au video zao bila ridhaa,” amesema kwa uchungu.
Ameongeza kuwa usambazaji wa kanda chafu unaosababishwa na mizozo ya kimapenzi au visasi umeendelea kuwa chanzo kikuu cha unyanyasaji, akisisitiza kuwa makosa hayo ni dhulma kamili ya kijinsia.
“Haya sio matani, sio mchezo. Ni ukatili unaoharibu maisha ya watu kimwili, kiakili na kijamii,” amesema.

Katika kusisitiza msimamo wa mashirika ya haki za wanawake na vijana, Janet Molo alitoa onyo kali kwa wote wanaohusika na vitendo hivyo, akisema kuwa sheria za Kenya, zikiwemo zile za Mtandao na Makosa ya Kijamii (Computer Misuse and Cybercrimes Act) na Sheria ya Dhulma za Kijinsia, zinaweka adhabu kali kwa wanaokutwa na hatia.
“Hakuna aliye juu ya sheria. Yeyote atakayepatikana akijihusisha na uvujaji wa kanda chafu atachukuliwa hatua kali bila kusita,” amesisitiza.
Aidha, Molo amehimiza jamii nzima kubeba wajibu wa kulinda hadhi ya kila mtu katika mitandao. Ameeleza kuwa wazazi na walezi wana jukumu muhimu la kuwafundisha watoto kuhusu usalama wa kimtandao, huku walimu na viongozi wakitakiwa kuongoza kampeni za uhamasishaji dhidi ya tabia za udhalilishaji mtandaoni. “Dhulma za kijinsia mtandaoni haziwezi kupigwa vita na mtu mmoja. Ni lazima tutangaze vita ya kitaifa dhidi ya uovu huu,” amesema.
Katika hafla hiyo, vijana walipata nafasi ya kujadili changamoto wanazokutana nazo mtandaoni, ambapo wengi walieleza kuwa ukosefu wa maarifa ya kisheria na ukosefu wa mifumo ya kuripoti mara nyingi huwafanya waathiriwa kunyamaza. Janet Molo ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa serikali na wadau kuimarisha vituo vya usaidizi wa waathiriwa ili kuhakikisha wanaopitia ukatili huu wanapata msaada wa kisheria, ushauri nasaha na ulinzi wanaohitaji.
Maadhimisho haya ya Siku 16 za Uhamasishaji yameashiria mwanzo wa kampeni ya kina katika maeneo ya Pwani, ambapo mashirika mbalimbali yameahidi kufanya warsha, midahalo ya vijana, na kampeni za mitandaoni ili kuzidisha uelewa kuhusu madhara ya dhulma za kijinsia mtandaoni. Janet Molo amehitimisha kwa kusisitiza kuwa jamii inapaswa kuchukua hatua mapema badala ya kusubiri madhara yatokee. “Ulimwengu wa dijitali ni mzuri, lakini pia unaweza kuwa sumu. Ni jukumu letu kuhakikisha unakuwa salama kwa wote,” amesema.
NA HARRISON KAZUNGU.