MUUNGANO WA WALIMU WA SEKONDARI ZA MSINGI WATAKA UHURU WA KUJISIMAMIA
By Dayo Radio
Published on 01/09/2025 17:43
News

Muungano wa walimu wa shule za sekondari za msingi nchini (KEJUSTA) umetaka serikali kupitia Wizara ya Elimu kuwapa uhuru na mamlaka ya kujisimamia shughuli zao pasi kuhitilafiwa na usimamizi wa shule za msingi.

 

Viongozi wa muungano huo, wakizungumza mjini Mombasa chini ya uongozi wa mwenyekiti wao James Odhiambo, wamesema walimu wa sekondari za msingi wametengwa na kudhulumiwa na mfumo wa sasa wa usimamizi.

 

"Walimu wa sekondari ya msingi wametengwa na usimamizi wa shule za msingi na sasa pana haja ya wao kutambuliwa kama muungano huru," amesema Odhiambo.

 

Ameongeza kuwa walimu wakuu wa shule za msingi bado ndio wanaosimamia bajeti na shughuli za shule za sekondari za msingi pamoja na zile za shule za msingi, hali inayotenga walimu wa sekondari za msingi.

 

Kwa upande wake, mwekahazina wa muungano huo, Juma Jigi, amesema mfumo wa sasa wa usimamizi wa shule za sekondari za msingi umekuwa kikwazo kwa walimu hao kuendeleza taaluma zao.

 

"Kulingana na jinsi taratibu za usimamizi wa shule za sekondari ya msingi ulivyo, inakuwa vigumu walimu hao kupandishwa cheo licha ya kwamba baadhi yao wamehitimu," amesema Jigi.

 

Wito wa muungano huo unakuja wakati ambapo sintofahamu inaendelea kugubika usimamizi wa shule za sekondari za msingi huku kitendawili cha mfumo wa uongozi kikiendelea kuwa kigumu kuteguliwa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!