Mwenyekiti mkuu wa shirika la AMKENI COMMUNITY Christine Kabuya, amewataka vijana wa Kaunti ya Mombasa kutumia talanta na vipaji walivyonavyo kama nyenzo vya kujikwamua kiuchumi badala ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wao wa kimaisha.
Akizungumza katika hafla ya maonyesho ya filamu ya uhamasisho wa masuala ya kijamii Bi:Kabuya ametaja kwamba kutokana na agizo la kamanda wa polisi wa ukanda wa pwani Ali Nuno la kuwapiga risasi na kuwauwa vijana wanaojihusisha na uhuni sasa hakuna njia nyengine ya kutumia isipokuwa kuwakomboa vijana kupitia talanta walizonazo.
Hata hivyo amesema kuwa shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya stadi za maisha, ujasiriamali, pamoja na ukuzaji wa vipaji mbalimbali ikiwemo sanaa, michezo na ufundi.
Aidha amebainisha kuwa hadi sasa vijana 200 tayari wamenufaika moja kwa moja na mpango huo, huku wengi wao wakianzisha miradi midogomidogo inayowaingizia kipato na kusaidia familia zao.
“Tunaamini kila kijana ana kipaji cha kipekee ambacho kinaweza kumuinua kimaisha. Badala ya kupoteza muda na nguvu kwenye uhalifu au makundi yasiyofaa, ni muhimu watumie talanta zao kujitengenezea ajira na kujenga maisha bora,” amesema Kabuya.
Wakati uo huo mwenyekiti huyo ametoa wito kwa viongozi wa serikali ya kaunti ya Mombasa kuweka mikakati madhubuti ya ugavi wa rasilimali na kuanzisha mifumo itakayowawezesha vijana kupata mitaji, mafunzo zaidi na masoko ya bidhaa zao huku akisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana ni uwekezaji wa maendeleo ya jamii nzima.
“Serikali ikiweka mkazo katika kuwaunganisha vijana kwenye vikundi na kuwapatia rasilimali, wataweza kushirikiana, kubuni miradi ya pamoja na kujiletea maendeleo endelevu,” ameongeza.
Kwa upande wake David Tembo mmoja wa vijana walionufaika na mradi huo, amesifia hatua hiyo akisema umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yake na vijana wengine waliopata mafunzo.

Tembo amesema kupitia mafunzo aliyoyapata, ameweza kuanzisha shughuli ndogondogo zinazomwingizia kipato na pia kuwashauri vijana wenzake kuhusu umuhimu wa kujitegemea.
“Mafunzo niliyopata yamenisaidia sana mashinani. Sasa nina ujuzi wa kutatua changamoto ndogondogo za kibiashara na hata kusaidia wengine kuanzisha miradi yao.Mradi huu umenifungua macho na kunipa matumaini mapya ya maisha,” amesema Tembo.
NA HARRISON KAZUNGU.