Kamati Kuu ya Bunge la Kitaifa ya Uchumi Samawati na Masuala ya Baharini imekutana na wadau mbalimbali kutoka sekta ya uvuvi katika Kaunti ya Mombasa kwa lengo la kujadili changamoto na masuala yanayowakumba wavuvi pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo.
Kikao hicho cha umma kilichoandaliwa mjini Mombasa kimekuwa sehemu ya mashauriano kuhusu mswada wa Usimamizi na Maendeleo ya Uvuvi uliopendekezwa bungeni na Kiongozi wa Wengi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni mbunge wa Marakwet Mashariki, Bowen David Kangogo, amesema kuwa mswada huo umelenga kuboresha mfumo wa kisheria wa sekta ya uvuvi.
"Mswada huu unalenga kutoa mfumo mpana wa kisheria kwa ajili ya usimamizi, maendeleo, uhifadhi wa uvuvi pamoja na rasilimali za majini kama njia mojawapo ya kuboresha na kurahisisha shughuli za uvuvi na masuala ya baharini," amesema Kangogo.
Katika kikao hicho, wavuvi walieleza malalamiko yao kuhusu kuenea kwa uvuvi haramu unaochochewa na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uvuvi, hali ambayo imetatiza shughuli zao baharini.
Mbunge wa Malindi, Amina Laura Mnyazi, ameitaka serikali kuweka mikakati ya kusaidia wavuvi kwa kuidhinisha vifaa bora vya uvuvi.
"Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi na Masuala ya Baharini inapaswa kutoa sera madhubuti ambazo zitaidhinisha vifaa vifaavyo vya uvuvi," amesema Mnyazi.
Wavuvi pia walilalamikia ushuru wa juu wanaotozwa kwa vifaa na biashara zao, pamoja na uhaba wa vifaa vya kisasa vinavyohitajika ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi.
"Tunapata hasara kubwa kwa sababu ya ushuru wa juu na ukosefu wa vifaa vya kisasa. Hali hii inatufanya tushindwe kushindana na wavuvi haramu ambao wanatumia mbinu za kisasa."
Kwa upande wake, kamati hiyo imewahakikishia wadau kwamba maoni yao yatajumuishwa kwenye ripoti itakayowasilishwa bungeni kabla ya kupitishwa kwa mswada huo, ili kuhakikisha sauti za wavuvi na wadau wengine wa sekta zinazingatiwa ipasavyo.
NA HARRISON KAZUNGU.