ISK YAPINGA SERA ILIYOPENDEKEZWA KUHUSU UTHAMINI WA MALI ZA UMMA.
By Dayo Radio
Published on 27/08/2025 15:30
News

Chama cha masoroveya humu nchini (Institution of Surveyors of Kenya – ISK) kimepinga vikali sera iliyopendekezwa na wizara ya fedha kuhusu uthamini wa mali za umma, kikisema kuwa hatua hiyo inahatarisha hatua za uthamini na usimamizi bora wa rasilimali za taifa.

 

Ikumbukwe kuwa hivi majuzi, wizara ya fedha ilitangaza kuanza kwa mikutano ya ukusanyaji maoni ya wananchi kuanzia tarehe 1 Septemba 2025.

 

Hata hivyo, chama hicho kimesema kuwa sera hiyo iliyopendekezwa haifati sheria ya wathamini (Cap 532) pamoja na viwango vya kitaifa na kimataifa vya uthamini ikiwemo Kenya Valuation Standards 2021 na ile ya International Valuation Standards 2025.

 

Kwa mujibu wa ISK, uthamini wa mali ni kazi ya kitaaluma inayopaswa kufanywa na wathamini waliobobea na kusajiliwa kisheria.

 

Chama hicho aidha kimeonya kuwa kuwaruhusu watu wasio na taaluma maalum kushiriki katika mchakato wa uthamini kutasababisha udanganyifu mkubwa na hata utoaji wa raslimali zisizo sahihi na hatimaye kupotea kwa mali za umma.

 

Aidha, ISK imelaani pendekezo la kuundwa kwa bodi mpya ya kusimamia mali za umma, ikisema kuwa hatua hiyo italeta mgongano wa majukumu na Bodi ya Usajili wa wathamini ambayo tayari ina mamlaka ya kudhibiti taaluma hiyo nchini.

 

Chama hicho kimependekeza kuwa badala ya kuendeleza sera hiyo, serikali iunde kikosi kazi cha wadau wakuu wakiwemo Chama cha masoroveya, Bodi ya Usajili wa wathamini, wizara ya Ardhi, Tume ya Kitaifa ya Ardhi na taasisi za elimu ya juu ili kuhakikisha sera ya uthamini wa mali za umma inazingatia sheria zilizopo na viwango bora vya kimataifa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!