Jumamosi ilikuwa siku yenye msisimko mkubwa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya matokeo makubwa na ya kushangaza kutokea viwanjani.
Tottenham Hotspur waliendelea kuwa mwiba kwa Manchester City baada ya kuibuka na ushindi wa 2–0 ugenini kwenye Etihad Stadium. Mabao ya Brennan Johnson na João Palhinha yaliwapa Spurs alama tatu muhimu, huku City wakipoteza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Katika Emirates Stadium, Arsenal walionesha ubabe mkubwa kwa kuichapa Leeds United 5–0. Jurrien Timber alifunga mabao mawili, huku Bukayo Saka akiongeza jingine kabla ya kuondoka uwanjani kutokana na majeraha. Mshambuliaji mpya Viktor Gyökeres alionyesha makali kwa kufunga mara mbili, akiwasha moto mbele ya mashabiki wa Gunners.

Brentford nao walisherehekea ushindi wao wa kwanza wa msimu baada ya kuilaza Aston Villa 1–0 kupitia bao la Dango Ouattara aliyefunga kwenye mechi yake ya kwanza. Kwa upande mwingine, Aston Villa wamesalia bila ushindi wala bao msimu huu, jambo linaloongeza presha kwa kikosi chao.

Katika Vitality Stadium, Bournemouth waliibuka na ushindi wa 1–0 dhidi ya Wolves shukrani kwa bao la mapema la Marcus Tavernier. Wolves walipoteza mchezaji mmoja kwa kadi nyekundu, na hali hiyo iliwapa Bournemouth nafasi ya kulinda alama tatu.
Burnley walipata alama zao za kwanza msimu huu baada ya kuifunga Sunderland 2–0 katika uwanja wa Turf Moor. Mabao kutoka kwa Josh Cullen na Anthony yalihakikisha kikosi hicho kinapata ushindi wa kifahari nyumbani.

Kwa ujumla, ilikuwa siku ya mshangao na burudani,Tottenham wakiendelea kuisumbua Man City, Arsenal wakidhibitisha ubora wao wa ushambuliaji, huku Brentford, Bournemouth na Burnley wakipata matokeo muhimu kwenye mbio za mapema za ligi.