Arsenal wameanza kampeni ya Ligi Kuu ya England msimu wa 2025/26 kwa ushindi muhimu wa ugenini baada ya kuibwaga Manchester United 1–0 katika uwanja wa Old Trafford, Jumapili, Agosti 17, 2025.
Goli pekee la mchezo lilifungwa mapema dakika ya 13 kupitia beki mpya Riccardo Calafiori, aliyemalizia kwa kichwa mpira wa kona baada ya golikipa wa United, Altay Bayindir, kushindwa kuudhibiti. Makosa hayo yamezua mjadala mkubwa kwani kipa namba moja André Onana alikuwa fit lakini hakuanza mchezo.

Licha ya kupoteza, Manchester United walimiliki zaidi ya asilimia 60 ya mpira na walipiga mashuti zaidi ya 20 kuelekea lango la Arsenal, lakini hawakupata njia ya kumtungua kipa David Raya aliyefanya kazi ya ziada kuilinda timu yake. Mashambulizi kutoka kwa washambuliaji wapya Benjamin Sesko, Matheus Cunha, na Bryan Mbeumo yalishindwa kuzaa matunda kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Arsenal.
Kocha wa United, Ruben Amorim, alisema licha ya matokeo, timu yake ilionyesha ari na mapambano, huku akisisitiza kuwa wachezaji wapya watatoa mwendelezo mzuri msimu huu. Kwa upande wake, kocha wa Arsenal Mikel Arteta alisifu umoja na nidhamu ya wachezaji wake, akisema walijibu makosa kwa mshikamano na walihakikisha wanalinda ushindi mpaka dakika ya mwisho.

Matokeo haya yanaipa Arsenal mwanzo mzuri kwenye harakati za kusaka taji, huku yakiacha mashabiki wa Manchester United na maswali mengi kuhusu chaguo la mlinda mlango na hatma ya safu ya ushambuliaji.
Na: Boniface Ziro