Wafanyakazi katika kiwanda cha Chemelil wakiandamana kupinga kutwaliwa kwa kiwanda hicho na Kibos. Picha|Alex Odhiambo
Wafanyakazi kampuni ya sukari ya Chemelil wamegoma wakishinikiza kulipwa malimbikizo ya mishahara ya Sh1.5 bilioni, wakishtumu serikali kwa kuwasaliti kwa kuendeleza mchakato wa kukodisha viwanda vya sukari kwa wawekezaji wa kibinafsi kabla ya kutimiza ahadi za kifedha.
Mgomo huo ulianza Jumanne, ambapo shughuli zote za ukarabati kiwandani zilisitishwa kabisa.
Wafanyakazi wanasema serikali ilikiuka makubaliano ya Mei 2025 kupitia Mkataba wa Maelewano (MoU) ulioelekeza malipo yote kufanyika kabla ya ukodishaji.
Kulingana na James Agumbah, msemaji wa wafanyakazi, serikali imetoa ahadi zisizotekelezwa, huku Wizara ya Kilimo ikitajwa kama mhusika mkuu wa kuvunja makubaliano hayo.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kuondoka katika nyumba za kampuni kabla ya kila senti kulipwa. Tunamwomba Rais William Ruto kuingilia kati kuhakikisha MoU inatekelezwa ili mpito uwe wa amani,” alisema Agumbah.
Kulingana na MoU hiyo, serikali iliahidi kulipa mishahara, michango ya pensheni na makato ya lazima kabla ya Juni 2026.
Pia, wafanyakazi walitakiwa kuendelea kuhudumu kwa miezi 12 baada ya mpito, huku walioondoka wakifaidika na marupurupu ya kujiondoa kazini.
Lakini sasa, wafanyakazi wanadai hawajalipwa mishahara ya Julai 2025, huku notisi ya kuwafuta kazi ifikapo Oktoba 31, 2025 ikitolewa kwa wafanyakazi wa Chemelil, Muhoroni na Sony Sugar.
Meneja Mkuu wa Chemelil, Jacob Agoch, amesema wawekezaji tayari wako tayari kushirikiana na wafanyakazi, lakini ucheleweshaji wa mishahara kutoka kwa serikali unawazuia kuendelea na mpango wa mpito.
“Tumewekewa miezi sita kufanikisha mpito, lakini ukosefu wa mishahara umekwamisha shughuli zote. Tunaiomba serikali itimize wajibu wake,” alisema Agoch.
Wafanyakazi wa Muhoroni Sugar nao wanadai Sh1.8 bilioni wakisisitiza kuwa hawatakubali kufutwa kazi bila kulipwa haki zao.
Josphat Nyachae, mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi, alilalamika kuwa wafanyakazi na wastaafu hawajapokea mishahara wala mafao yao licha ya kutumikia kampuni kwa miaka mingi.
“Huu ni usaliti wa kiwango cha juu. Wengine hawana pesa za karo ya shule wala chakula. Serikali lazima ilipe kwanza,” alisema Nyachae.
Wengine kama Dixon Odero, aliyestaafu 2021, wamesema hawataondoka kwenye nyumba za kampuni hadi walipwe mafao yao kikamilifu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Kipronoh Ronoh, alielekeza wakurugenzi wa kampuni nne za sukari zinazosimamiwa na serikali kutoa notisi rasmi za kuwatimua wafanyakazi wote, ikiwa ni sehemu ya mpango wa ukodishaji kwa miaka 30 kwa wawekezaji binafsi.
Kampuni zilizoathiriwa ni Chemelil iliyokodishwa kwa Kibos Sugar, Muhoroni kwa West Valley Sugar, Nzoia kwa West Kenya Sugar na Mumias kwa Sarrai Group, ingawa mpango huo ulizuiliwa na mahakama.
Zaidi ya wafanyakazi 5,000 wanatarajiwa kuathirika, ambapo watakaoendelea kufanya kazi chini ya wawekezaji wapya watalazimika kuomba upya ajira.
Vyama vya wafanyakazi vimetishia kuitisha migomo mikubwa ya kitaifa iwapo serikali haitatimiza masharti ya MoU na kulipa madeni yote kabla ya Oktoba 31, 2025.