Kenya imepata ushindi wa thamani dhidi ya Zambia kwa goli 1–0 katika mchezo wa makundi wa michuano ya CHAN 2024 uliochezwa Jumapili, Agosti 17, 2025, katika uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani. Bao pekee la Harambee Stars lilifungwa na Ryan Ogam dakika ya 75 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa mchezaji aliyeingia kutoka benchi, Boniface Muchiri. Licha ya juhudi za mlinda mlango wa Zambia, Charles Kalumba, kudhibiti mashambulizi kadhaa ya Kenya, Ogam alihakikisha mpira unatinga wavuni na kutoa furaha kubwa kwa mashabiki waliokuwepo uwanjani.
Kwa matokeo hayo, Kenya imemaliza kileleni mwa Kundi A bila kupoteza mchezo wowote, ikijiunga na Morocco katika hatua ya robo-fainali. Wakati huo huo, Zambia imeondolewa kwenye mashindano baada ya kushindwa kupata hata pointi moja. Ushindi huu umeongeza morali ya Harambee Stars, ambao sasa wanajiandaa kukutana na Madagascar katika hatua inayofuata, huku Morocco ikitarajiwa kumenyana na Tanzania.

Mchezo huu pia ulikuwa na mvuto mkubwa nje ya uwanja. Tiketi zote 27,000 za pambano hili ziliuzwa kwa muda mfupi mno, na CAF ililazimika kupunguza idadi ya mashabiki kutokana na changamoto za usalama. Kwa mashabiki waliokosa nafasi ya kuingia Kasarani, serikali na FKF waliandaa fanzones rasmi katika maeneo kadhaa ya Nairobi ikiwemo Uhuru Park, Dandora Stadium na Jacaranda Grounds, ambapo mashabiki waliweza kushuhudia mechi kupitia skrini kubwa kwa usalama.

Kwa ujumla, ushindi huu wa Harambee Stars si tu ulihakikisha nafasi yao katika robo-fainali, bali pia umeonyesha dalili ya kikosi kipya kinachoweza kushindana na wapinzani wakubwa barani Afrika
Na: Boniface Ziro