Tottenham Hotspur wameanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya England kwa kishindo baada ya kuwachapa Burnley mabao 3–0 katika mechi iliyochezwa Jumamosi, Agosti 16, 2025. Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha mpya Thomas Frank, ambaye alipata ushindi wa kuvutia kwenye mchezo wake wa ufunguzi. Nyota wa Brazil, Richarlison, aliibuka shujaa kwa kufunga mabao mawili mazuri, huku Brennan Johnson akihakikisha alama tatu zinasalia kwa Spurs kwa goli la tatu.

Mchezaji mpya aliyejiunga na Spurs msimu huu, Mohammed Kudus, alionyesha ubora wake mara moja kwa kutoa pasi mbili za mabao, zote zikimsaidia Richarlison kutupia wavuni. Kudus alipongezwa sana na mashabiki waliomshangilia kwa uchezaji wake wa ubunifu na mchango wake mkubwa uwanjani.
Kwa upande wa Burnley, kulikuwa na kisa cha kipekee baada ya kipa wao Martin Dúbravka kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi Kuu kuadhibiwa chini ya kanuni mpya ya sekunde nane, inayomtaka mlinda mlango kuachia mpira haraka. Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa lakini pia liliwaweka Burnley kwenye wakati mgumu mapema kwenye mchezo.

Kwa ujumla, Spurs walitawala mpira kwa asilimia kubwa, wakashambulia kwa kasi na nidhamu, na wakionyesha kuwa wako tayari kupambana vikali msimu huu. Mashabiki pia walitoa sapoti kubwa kwa Mathys Tel, ambaye hivi karibuni amekuwa akilengwa na maneno ya kibaguzi. Ushindi huu unaonyesha mwanzo mpya wenye matumaini chini ya Thomas Frank, huku Tottenham ikilenga kuwa miongoni mwa washindani wakuu msimu huu.
Mwandishi: Boniface Ziro