KENYA YAITANDIKA CHAD 2-1 KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI – USHINDI WA KWANZA CHINI YA KOCHA BENNI MCCARTHY
By Dayo Radio
Published on 11/06/2025 12:26
Sports

Kenya imepata ushindi wa kihistoria dhidi ya Chad kwa mabao 2-1 katika mechi ya pili ya kirafiki iliyochezwa tarehe 10 Juni 2025 huko Marrakech, Morocco. Ushindi huu unakuja siku chache baada ya sare tasa ya 0-0 kati ya timu hizo mbili mnamo Juni 7, na umeashiria ushindi wa kwanza kwa kocha mpya wa Harambee Stars, Benni McCarthy, tangu aanze kuifundisha timu hiyo mapema mwaka huu.

Katika mchezo huo wa pili, Emmanuel Osoro alifungua ukurasa wa mabao kwa Kenya kwa kupachika bao la kwanza dakika ya 18. Kenya iliendelea kushambulia kwa kasi, na kufikia dakika ya 44, David Sakwa aliongeza bao la pili baada ya kutumia makosa ya safu ya ulinzi ya Chad. Chad walijibu kipindi cha pili kupitia kwa Ali Mahamat Adam aliyefunga bao dakika ya 60, lakini juhudi zao hazikuweza kuwazuia Harambee Stars kuibuka na ushindi.

Kocha Benni McCarthy alifanya mabadiliko makubwa kwa kufanya mabadiliko tisa kwenye kikosi kilichocheza mechi ya kwanza, jambo lililosaidia kuleta nguvu mpya na nidhamu uwanjani. Miongoni mwa waliong’aa ni kipa Farouk Shikhalo ambaye alifanya kazi ya ziada kuzuia mashambulizi ya Chad hasa kipindi cha pili.

Ushindi huu umeleta matumaini mapya kwa mashabiki wa soka nchini Kenya, hasa wakati huu ambapo timu inaendelea kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa michuano ya CHAN 2025 na Kombe la Dunia la FIFA 2026. Pia, ushindi huu umetamatisha mfululizo wa mechi sita bila ushindi kwa Harambee Stars, na kuwaweka katika nafasi nzuri ya kujiamini na kujenga timu thabiti chini ya uongozi wa McCarthy. Wakati huo huo, Chad wanaendelea kusaka ushindi wao wa kwanza tangu Machi 2024.

 

By: BekaSmasher

Comments
Comment sent successfully!