MSIMU WA EPL WAKAMILIKA: LIVERPOOL WASHINDA TAJI, TIMU TATU ZASHUKA DARJA
By Dayo Radio
Published on 26/05/2025 10:46
Sports

Msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu ya England (EPL) ulikamilika rasmi Jumapili, Mei 25, 2025, kwa raundi ya mwisho (Matchday 38) iliyojawa na msisimko, ushindani mkali, na matukio ya kihistoria. Liverpool walitwaa ubingwa kwa alama 84 licha ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Crystal Palace, na hivyo kunyakua taji lao la kwanza tangu msimu wa 2019/20. Arsenal walimaliza nafasi ya pili kwa pointi 74 baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Southampton, ushindi uliowapa rekodi mpya ya ushindi 14 mfululizo kwenye mechi za mwisho ya msimu—rekodi ambayo haikuvunjwa kwa zaidi ya karne moja.

Manchester City walimaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi 71 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham, huku Ilkay Gündogan akifunga kwa bicycle kick ya kuvutia na Kevin De Bruyne akiingia dakika ya 83 katika mechi yake ya mwisho kwenye EPL akiwa na City. Chelsea waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Nottingham Forest kupitia bao la Levi Colwill, na kumaliza katika nafasi ya nne kwa pointi 69. Newcastle United walimaliza wa tano kwa pointi 66 licha ya kupoteza 1-0 dhidi ya Everton, lakini waliwazidi Aston Villa kwa tofauti ya mabao. Villa walifungwa 2-0 na Manchester United na kumaliza katika nafasi ya sita. Nottingham Forest walimaliza wa saba kwa pointi 65 na watashiriki UEFA Conference League.

Kwa upande wa kushuka daraja, Leicester City (nafasi ya 18, alama 25), Ipswich Town (nafasi ya 19, alama 22), na Southampton (nafasi ya 20, alama 12) zimeshushwa hadi ligi ya Championship. Mechi ya mwisho pia ilishuhudia nyota kadhaa wa soka wakiagana rasmi, akiwemo Kevin De Bruyne wa Manchester City, aliyepewa heshima na mashabiki wa klabu hiyo. Vilevile, Gary Lineker alitangaza rasmi kustaafu uwasilishaji wa kipindi cha Match of the Day baada ya miaka 25.

Comments
Comment sent successfully!