Peter Mwaniki Maina mwenye umri wa miaka 47 na baba wa watoto wanne, amejishindia shilingi milioni 102 kupitia SportPesa Mega Jackpot baada ya kubashiri kwa usahihi matokeo ya mechi zote 15.Mwaniki ambaye amefanya kazi ya udereva wa malori kwa takriban miaka 20 alisema ushindi huo utampa fursa ya kuboresha maisha ya familia yake na kuimarisha usalama wao wa kifedha.
Akizungumza wakati wa kutambulishwa rasmi mjini Mombasa, Mwaniki alisema hana mpango wa kufanya maamuzi ya haraka kuhusu matumizi ya fedha hizo.
“Kwa sasa sina mipango yoyote ya haraka kuhusu matumizi ya fedha hizi. Nimepata Ushindi huu bila kutarajia, hivyo sitaki kufanya maamuzi ya pupa na nitaendelea na kazi yangu ya udereva nikiendelea kufikiria kwa kina,” alisema Mwaniki.

Kwa upande wake Afisa wa Mawasiliano wa kampuni ya SportPesa Willis Ojwang, alisema kampuni hiyo itamunganisha Mwaniki na wataalamu wa masuala ya fedha watakaomsaidia kupanga na kutumia fedha hizo kwa busara.
Ojwang alisema lengo ni kuhakikisha kuwa fedha hizo zinamnufaisha Mwaniki pamoja na familia yake kwa muda mrefu.
“Nia yetu kubwa ni kuhakikisha kuwa fedha hizi zinamnufaisha Mwaniki pamoja na familia yake. Kuanzia wiki ijayo, tutamunganisha na wataalamu wa masuala ya fedha ili wamshauri jinsi ya kutumia fedha hizo kwa ubora zaidi ,” alisema Ojwang.

Ikubukwe kuwa Peter Mwaniki ndiye mshindi wa kwanza wa SportPesa Mega Jackpot mwaka huu, huku Caroline Nyakundi na Gaudencia Sella wakijishindia bonasi za shilingi milioni 2.19 na milioni 3.5 mtawalia.

Ushindi huo unaendeleza historia ya SportPesa Mega Jackpot, shindano la kubashiri matokeo ya soka linalowapa washiriki nafasi ya kujishindia zawadi kubwa kwa kutabiri kwa usahihi matokeo ya mechi zote zinazoshindaniwa.
