WAKAZI WA PWANI WAPINGA MPANGO WA KUVUNJWA KWA CDA
By Dayo Radio
Published on 24/10/2026 21:06 • Updated 24/10/2026 21:07
News

Wakazi wa Ukanda wa Pwani wamepinga pendekezo la Serikali la kuvunja Mamlaka za Maendeleo za Kikanda, wakitaka taasisi hizo zifanyiwe mageuzi na kuimarishwa badala ya kuvunjwa kabisa.

Wakazi hao wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Smart Move Community Jamal Abdallah Kidyogo wamewataka wabunge kusitisha mpango wa kuvunjwa kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Pwani (CDA), pamoja na mamlaka nyingine tano za kikanda, na badala yake kuharakisha utekelezaji wa mfumo wa mageuzi uliopendekezwa mwaka 2023.

"Pwani haihitaji kupunguzwa kwa uratibu wa maendeleo, bali inahitaji taasisi imara, za kisasa na zinazowajibika ili kuendeleza mipango ya maendeleo ya kikanda,” alisema Jamal Abdallah.

Wakazi hao pia walilalamikia muda mfupi uliotolewa kwa ushiriki wa umma, wakitaka mikutano zaidi kufanyika katika kaunti zote zilizoathiriwa na nyaraka muhimu kutafsiriwa katika lugha za wenyeji.

Walisema wananchi wanapaswa kupewa muda na taarifa za kutosha ili kutoa maoni kuhusu maamuzi yanayoweza kuathiri mustakabali wa maendeleo ya eneo lao.

“Wananchi katika kaunti zilizoathiriwa wanapaswa kupewa muda wa kutosha na taarifa muhimu ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutoa maoni kuhusu mswada huu wenye athari kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya maeneo yao.” Alisema Jackline Kitutu.

Kwa upande wake Mohamed Ali Mwachausa alisisitiza kwamba wananchi wanapaswa kupewa muda na taarifa za kutosha ili kutoa maoni kuhusu maamuzi yanayoweza kuathiri mustakabali wa maendeleo ya eneo lao, akiongeza CDA inaendesha miradi mbali Mbali Pwani.

 “Hatuwezi kufanya maamuzi yenye tija bila kupewa muda wa kutosha na taarifa sahihi.Tunataka ushiriki wa umma uwe wa maana, jumuishi na uwafikie wananchi wote katika kaunti zilizoathiriwa, ili sauti zao zisikike kabla ya maamuzi yatakayogusa mustakabali wa maendeleo ya maeneo yetu kufanywa Bungeni.” Alisema Ali Mwachausa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, Bw. Joseph Tunje, alisema CDA inapaswa kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha mipango ya kikanda, kuvutia uwekezaji na kuratibu miradi ya pamoja bila kuingilia majukumu ya serikali za kaunti.

 “Tunachohitaji ni kuimarisha ushirikiano baina ya kaunti na kufafanua upya majukumu ya CDA ili ijikite katika mipango ya kikanda, kuvutia uwekezaji na kuratibu maendeleo kwa namna inayokamilisha majukumu ya serikali za kaunti,” alieleza Joseph Tunje.

Akijibu hoja hizo, mbunge wa Ganze Kazungu Tungule na Mbunge wa Banissa Ahmed Maalim Hassan, waliwahakikishia wananchi kuwa maoni yao yatazingatiwa katika kuandaa ripoti ya kamati kwa Bunge.

 “Tunawashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yenu kuhusu mswada huu. Nawahakikishia kuwa tutawasilisha maoni mliyotupatia tutakapokutana kuandaa ripoti yetu na matakwa yenu yatazingatiwa Kikamilifu,” alisema Kazungu Tungule.

Kamati hiyo ilitembelea Hospitali Ndogo ya Malindi kukagua maendeleo ya ujenzi wa vitengo vya wagonjwa mahututi (ICU) na wanaohitaji uangalizi wa karibu (HDU), vinavyoendelezwa kwa ushirikiano wa CDA na Serikali ya Italia, pamoja na mradi wa barabara ya Mjanaheri–Ngomeni.

Comments
Comment sent successfully!