MAFUNZO YA UFUNDI YATAIMARISHA USALAMA MOMBASA.
By Dayo Radio
Published on 14/10/2026 20:54
News

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Mohammed Noor Hassan, amesema kuwa mpango wa serikali wa kuwapa vijana mafunzo ya ufundi na kuwaunganisha na fursa za ajira utasaidia kupunguza visa vya uhalifu na kuimarisha usalama katika Kaunti ya Mombasa na ukanda wa Pwani kwa ujumla.

 

Akizungumza mjini Mombasa wakati wa hafla iliyoandaliwa chini ya mpango wa NGAO, Noor amesema kuwa mafunzo hayo yatawapa vijana fursa ya kujiongezea ujuzi, kujiendeleza kielimu na kujiandaa kwa soko la ajira, hatua inayoweza kuwasaidia kujiepusha na vitendo vya uhalifu na makundi ya kihalifu.

 

Kamishna Noor amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa zinazotolewa na serikali kujiendeleza badala ya kutegemea shughuli za usafirishaji wa abiria kwa pikipiki za boda boda pekee.

 

“Tunataka vijana wetu wawe na ujuzi, waweze kujiajiri na kupata ajira katika miradi mikubwa ya maendeleo. Vijana wanapaswa kutumia fursa hizi kujenga maisha yao badala ya kujiingiza katika makundi ya kihalifu,” asema Noor.

 

Kamishna huyo ameeleza kuwa baada ya kupata mafunzo na ujuzi unaohitajika, vijana watakuwa katika nafasi nzuri ya kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na miradi mikubwa ya serikali, ikiwemo Mradi wa Mafuta wa Lamu, Eneo Maalumu la Kiuchumi la Dongo Kundu na Eneo Maalumu la Kiuchumi la Vipingo.

 

Amesistiza kuwa miradi hiyo inatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na ajira, hivyo vijana wanapaswa kujiandaa mapema kwa kupata ujuzi unaohitajika ili waweze kushindana na kunufaika na nafasi zitakazojitokeza.

 

“Usalama wa jamii haujengwi kwa juhudi za vyombo vya usalama pekee. Kuwapa vijana ujuzi, fursa za kujiajiri na ajira ni sehemu muhimu ya kuwakinga dhidi ya vishawishi vya uhalifu,” a

 

Noor amewahimiza vijana ukanda wa pwani kuchangamkia mipango ya mafunzo ya ufundi na miradi ya maendeleo inayolenga kuwawezesha kiuchumi, akibainisha kuwa uwezeshaji wa vijana ni hatua muhimu katika kujenga jamii yenye usalama na maendeleo endelevu.

 

Na Peter Mbonge.

Comments
Comment sent successfully!