WABURUNDI WAFURIKA UBALOZI NAIROBI KUFUATIA TAHARUKI YA WAFANYABIASHARA WA KIGENI
By Dayo Radio
Published on 09/09/2026 11:54
News

Mamia ya raia wa Burundi wanaoishi Kenya wamefurika katika Ubalozi wa Burundi, ulioko Kilimani jijini Nairobi, wakitafuta nyaraka za kusafiria na msaada wa kurekebisha hadhi yao ya kisheria. Baadhi yao wameonekana wakiwa na mizigo na wakisubiri huduma kwa muda mrefu, huku wengine wakisema wanajiandaa kurejea nchini Burundi kutokana na hofu iliyotokana na hatua za serikali dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kutoa maelekezo ya kudhibitiwa biashara ndogo ndogo zinazoendeshwa na wageni bila vibali na leseni zinazohitajika. Serikali imesisitiza kuwa hatua hizo hazilengi kuwafukuza raia wa nchi jirani, bali kudhibiti biashara ndogo ndogo na kulinda fursa za Wakenya. Hata hivyo, kumekuwa na taarifa za baadhi ya raia wa Burundi kukabiliwa na vitisho na unyanyasaji, hali iliyoongeza hofu miongoni mwa jamii hiyo.

Kwa upande wake, Serikali ya Kenya imeanzisha dirisha maalum la usajili na uandikishaji wa raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wasio na nyaraka kamili, wakiwemo Waburundi. Msemaji wa Serikali, Charles Owino, amesema wale wanaojitokeza kwenye mchakato huo watachukuliwa kuwa nchini kihalali wakati wa kipindi cha usajili.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’oei, ametembelea ubalozi huo na kuomba radhi kwa Waburundi waliodai kukumbwa na unyanyasaji, huku akiahidi hatua za kuimarisha usalama wao.

Wakati uo huo, Ubalozi wa Burundi umeanza kuwezesha raia wake wanaotaka kurejea nyumbani kupata nyaraka za kusafiria za Laisser-Passer. Taarifa ya ubalozi inaonyesha kuwa hati hiyo hutumika kusafiria ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ina uhalali wa mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa UNHCR, Kenya inawahifadhi takriban wakimbizi na waomba hifadhi 16,000 kutoka Burundi, ingawa idadi ya Waburundi  wanaoishi na kufanya kazi nchini ni zaidi.

Comments
Comment sent successfully!