KENYA AIRWAYS YAATHIRIWA NA HITILAFU YA MFUMO WA TRAFIKI YA ANGA UINGEREZA
By Dayo Radio
Published on 09/09/2026 11:44
News

Shirika la ndege la Kenya Airways limeathiriwa na hitilafu ya kiufundi katika mfumo wa National Air Traffic Services, NATS, nchini Uingereza. Hitilafu hiyo ya tarehe nane Septemba imesababisha usumbufu mkubwa wa safari za ndege, huku zaidi ya safari elfu moja zikighairiwa na mamia ya ndege kuchelewa katika viwanja mbalimbali, ikiwemo Heathrow na Gatwick.

Ndege ya Kenya Airways, KQ100, iliyokuwa ikitoka Nairobi kuelekea London, iliathiriwa na hali hiyo na kuelekezwa katika Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris, Ufaransa, kabla ya kuendelea na safari kuelekea London Heathrow. Hatua hiyo ilitokana na vizuizi vya muda vilivyowekwa katika anga ya Heathrow kufuatia hitilafu hiyo.

Kwa upande mwingine, safari ya KQ101 kutoka London Heathrow kuelekea Nairobi iliathiriwa na usumbufu huo. Hata hivyo, taarifa zilizopatikana hazithibitishi kwamba safari hiyo ilighairiwa, hivyo abiria wanashauriwa kuthibitisha hali ya safari zao moja kwa moja na Kenya Airways kabla ya kuelekea uwanjani.

 Kufikia sasa NATS imetangaza kuwa hitilafu hiyo imetatuliwa,ila usumbufu unaendelea kwa muda kutokana na ndege, wafanyakazi na abiria kuwa katika maeneo tofauti. Abiria wa Kenya Airways wameshauriwa kufuatilia taarifa za shirika hilo na kuwasiliana nalo kwa maelezo kuhusu mipango mbadala ya safari.

Comments
Comment sent successfully!