Serikali imeendeleza vita dhidi ya dawa za kulevya na pombe haramu nchini, huku shehena ya metheni yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.2 ikiteketezwa katika Kiwanda cha Bamburi Cement, Mombasa.
Waziri wa usalama wa Ndani na utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, ameongoza zoezi hilo la uteketezaji wa dawa hizo, akisema hatua hiyo ni ishara ya mipango ya Serikali ya kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na kulinda jamii dhidi ya madhara yanayotokana na matumizi ya mihadarati.
Shehena hiyo iliyoteketezwa ilikuwa na zaidi ya kilo 1,000 za metheni ambayo ilikamatwa mwezi Oktoba mwaka 2025 katika Bahari ya Hindi na kikosi cha pamoja cha taasisi za usalama.
Murkomen amesema operesheni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais William Samoei Ruto la kuimarisha vita dhidi ya dawa za kulevya na pombe haramu, ambazo zimekuwa tishio kwa familia na vijana nchini.

Hata hivyo amesema Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti biashara hiyo haramu, ikiwemo kuongeza ufuatiliaji katika mipaka ya nchi ili kuzuia dawa za kulevya kuingia au kupita nchini.
Aidha, amesema Serikali inalenga kuvunja mitandao ya watu wanaohusika na usafirishaji na usambazaji wa dawa hizo, huku ikifuatilia pia mali na fedha zinazotokana na biashara ya mihadarati.
Waziri huyo aidha amesema Serikali pia inaendelea kuziba mianya ya kisheria ambayo inaweza kutumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kukwepa mkono wa sheria.

Amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu wanaohusika moja kwa moja au kwa njia nyingine katika biashara ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa Serikali haitalegeza kamba katika operesheni hiyo.
“Hatutarudi nyuma hadi tutakapodhibiti janga hili ambalo linaharibu familia, kuharibu maisha ya vijana wetu na kuchochea uhalifu wa kupangwa,” Murkomen amesema.
Wakati huohuo amesema vita dhidi ya dawa za kulevya haviwezi kufanikiwa kwa juhudi za taasisi moja pekee, bali vinahitaji ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya usalama, taasisi za Serikali, jamii na washirika wa kimataifa.
Amezipongeza taasisi mbalimbali zilizoshiriki katika kukamatwa kwa shehena hiyo na kuhakikisha inafikia hatua ya kuteketezwa.

Miongoni mwa taasisi hizo ni National Police Service, Kenya Defence Forces, National Intelligence Service, NACADA, Financial Reporting Centre, Kenya Revenue Authority, Kenya Bureau of Standards, Anti-Counterfeit Authority, Assets Recovery Agency, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma pamoja na Kenya Coast Guard Service.
Murkomen amesema ushirikiano huo umewezesha Serikali kuimarisha ufuatiliaji na kukabiliana na mitandao ya kimataifa inayojihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia njia za baharini na mipaka ya nchi.
Ameeleza kuwa eneo la Bahari ya Hindi ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji uangalizi mkubwa kutokana na uwezekano wa kutumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha mihadarati kuelekea Kenya na mataifa mengine.
Kwa upande mwingine, Serikali imewatambua washirika wa kimataifa wanaosaidia Kenya katika vita hivyo, akiwemo United Nations Office on Drugs and Crime pamoja na Serikali ya Marekani.
Murkomen amesema ushirikiano wa kimataifa ni muhimu kutokana na ukweli kwamba biashara ya dawa za kulevya inahusisha mitandao inayovuka mipaka ya nchi.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mataifa na mashirika ya kimataifa katika kubadilishana taarifa za kiusalama, kufuatilia wasafirishaji wa dawa za kulevya na kuzuia mitandao hiyo kutumia Kenya kama njia ya kupitishia mihadarati.
Amesema pia Serikali inalenga kuwafuatilia wahusika wanaonufaika kifedha kutokana na biashara hiyo kupitia uchunguzi wa mali na fedha zinazodhaniwa kuwa zimepatikana kutokana na uhalifu.
Kwa mujibu wa Murkomen, hatua hiyo inalenga kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya havilengi tu kukamata na kuteketeza mihadarati, bali pia kuvuruga msingi wa kifedha unaowezesha mitandao hiyo kuendelea kufanya biashara.
Amesema Serikali inatambua madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na dawa za kulevya, hususan miongoni mwa vijana, ambao ndio walio katika hatari kubwa ya kuathiriwa na matumizi ya mihadarati.
Amesema matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuchangia kuvunjika kwa familia, kuharibu maisha ya vijana na kuongeza changamoto za uhalifu katika jamii.
Kwa msingi huo, Serikali imesisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Murkomen amesema hatua ya kuteketeza shehena hiyo ya methamphetamine yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.2 ni sehemu ya juhudi pana za Serikali za kukabiliana na dawa za kulevya kuanzia katika chanzo, njia za usafirishaji hadi kwa wasambazaji na wanufaika wa biashara hiyo.
Serikali imesema haitasitisha operesheni hizo na itaendelea kuimarisha usalama katika maeneo ya mipakani, bandari na Bahari ya Hindi ili kuzuia dawa za kulevya kusafirishwa kupitia Kenya.
Zoezi hilo la uteketezaji wa methamphetamine linajiri wakati Serikali ikiendelea kuweka msisitizo katika vita dhidi ya dawa za kulevya na pombe haramu, huku ikiahidi kuendeleza ushirikiano wa taasisi mbalimbali hadi pale tishio hilo litakapodhibitiwa.
NA HARRISON KAZUNGU.