KTDA YAZINDUA USAFIRISHAJI WA TANI 99,000 ZA MBOLEA KUPITIA SGR, YAOMBA RUZUKU KUWALINDA WAKULIMA WA CHAI.
By Dayo Radio
Published on 08/09/2026 16:58
News

Shirika la Maendeleo ya majani  chai nchini (KTDA) limeanza rasmi kusafirisha tani 99,000 za mbolea kutoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi kupitia reli ya Standard Gauge Railway (SGR), hatua inayolenga kuhakikisha zaidi ya wakulima wadogo 650,000 wa chai wanapata mbolea kwa wakati kabla ya msimu wa mvua za vuli.

Mbolea hiyo imewasili katika Bandari ya Mombasa Septemba 3, 2026, ikiwa ni mzigo wa kwanza kati ya meli tatu zinazotarajiwa kuwasili nchini mwezi huu.

Baada ya kufungashwa, tani hizo 99,000 zinatarajiwa kuzalisha takribani mifuko milioni 1.9 ya mbolea aina ya NPK, yenye uzito wa kilogramu 50 kila mmoja. Mbolea hiyo itasambazwa katika viwanda vya chai nchini kwa ajili ya kuwafikia wakulima.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo wa usafirishaji katika Bandari ya Mombasa, Mwenyekiti wa Kitaifa wa KTDA, Enos Njeru, EGH, amesema matumizi ya SGR yatawezesha mbolea kufikishwa Nairobi kwa ufanisi na kwa wakati.

“Usafirishaji wa mbolea kutoka Mombasa hadi Nairobi kwa reli unatoa kiungo bora na cha kuaminika kutoka bandarini,” amesema Njeru.

Aidha amesema baada ya mbolea kufika Nairobi, itasafirishwa kwa njia ya barabara hadi katika viwanda husika vya chai, ambako itatolewa kwa wakulima.

Njeru amesema KTDA inalenga kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati, hasa wakati nchi inapoelekea katika msimu wa mvua.

Wakati huo huo ameeleza kuwa KTDA hununua mbolea kwa wingi kupitia zabuni za kimataifa zenye ushindani, hatua inayowezesha shirika kutumia nguvu ya ununuzi wa pamoja na kupata bei shindani.

Kwa mujibu wa Njeru, kiwango cha mbolea kinachonunuliwa kimeongezeka kutoka tani 93,000 mwaka 2023 hadi tani 99,000 mwaka huu. Ongezeko hilo limechangiwa pia na mahitaji kutoka kwa wazalishaji wa chai ambao si wanachama wa KTDA na wanaotaka kunufaika na bei shindani inayopatikana kupitia ununuzi wa pamoja.

Hata hivyo, KTDA imeeleza wasiwasi kuhusu ongezeko kubwa la gharama ya mbolea kutokana na changamoto za kimataifa, ikiwemo migogoro ya Mashariki ya Kati, kupanda kwa bei ya gesi asilia, mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha na gharama za usafirishaji.

Njeru amesema bei ya mbolea hiyo imefika zaidi ya Sh5,500 kwa mfuko wa kilo 50, hali inayoweza kuongeza mzigo kwa wakulima wa chai.

Kwa miaka mitano iliyopita, wakulima wa chai wamekuwa wakinufaika na mpango wa serikali uliowawezesha kupata mfuko mmoja wa mbolea kwa bei ya Sh2,500, hatua iliyosaidia kuwalinda dhidi ya athari za kupanda kwa gharama za pembejeo katika soko la kimataifa.

KTDA sasa imeiomba serikali kuendeleza ruzuku hiyo mwaka huu ili kuwalinda wakulima wa chai dhidi ya ongezeko la gharama.

Njeru amesema wakulima wa mazao mengine wameahidiwa kupata mbolea kwa bei ya Sh2,000 kwa mfuko, hivyo ameitaka serikali kuhakikisha wakulima wa chai nao wanajumuishwa katika mpango huo.

“Tunaomba serikali iongeze ruzuku mwaka huu ili kuwalinda wakulima wetu wa chai. Wakulima wa mazao mengine wameahidiwa ruzuku itakayowezesha mfuko mmoja kuuzwa kwa Sh2,000, na tunaomba wakulima wa chai nao wapewe fursa hiyo,” amesema.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameitaka Wizara ya Kilimo kushughulikia malimbikizo ya fedha za ruzuku ya mbolea za miaka iliyopita, akisema madeni hayo yanaendelea kuwa mzigo kwa wakulima kutokana na gharama za riba.

“Ninaomba PS na maafisa wengine wa serikali waliopo kuhakikisha suala la malimbikizo ya ruzuku ya miaka iliyopita linashughulikiwa. Kiasi hicho kinaendelea kuwa mzigo kwa wakulima wa chai,” amesema Njeru.

Wakati huo huo, KTDA imewataka wakulima kuchukua mbolea mara tu itakapowasili katika viwanda vyao na kuitumia kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu kutoka kwa maafisa wa ugani.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mashamba ya chai yanaendelea kuwa na afya, huku ubora wa majani mabichi ukiimarishwa.

Hafla hiyo ya kuashiria kuanza kwa usafirishaji wa mbolea imehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Paul Rono; Afisa Mkuu Mtendaji wa Tea Board of Kenya, Willy Mutai; maafisa wa Kenya Ports Authority, wawakilishi wa Kenya Railways; pamoja na washirika wa usafirishaji wa Bultstream wakiongozwa na Ernest Ondego, pamoja na wakurugenzi na menejimenti ya KTDA.

 

NA HARRISON KAZUNGU

Comments
Comment sent successfully!