MVUA NYINGI KUTARAJIWA KUNYESHA OKTOBA HADI DISEMBA.
By Dayo Radio
Published on 07/09/2026 21:10
News

Msimu wa mvua za Oktoba hadi Desemba 2026 unatarajiwa kuwa na mvua nyingi kuliko kawaida katika Kaunti ya Mombasa, huku joto likitarajiwa kuwa juu kuliko wastani katika maeneo ya Pwani. 

Utabiri wa KMSA unaonyesha kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili hadi ya tatu ya Oktoba na kuendelea hadi wiki ya kwanza au ya pili ya Desemba. 

Kwa mujibu wa utabiri huo, msimu huu unaweza kushuhudia vipindi virefu vya mvua pamoja na mvua kubwa za hapa na pale, hali inayoweza kusababisha mafuriko katika maeneo ya mabondeni na sehemu zenye mifumo duni ya kupitisha maji.

Wakazi wa Mombasa wanashauriwa kuchukua tahadhari, ikiwemo kuepuka maeneo yanayokumbwa na mafuriko, kutotumia maji yaliyochafuliwa na maji ya mafuriko, pamoja na kuwa waangalifu wanaposafiri wakati wa mvua kubwa.

Aidha, wananchi wanashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa kutoka Idara ya Hali ya Hewa Kenya na mamlaka za kaunti, huku wakiweka mipango ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

Comments
Comment sent successfully!