FUNDI BORA KAZI BORA YAWAWEZESHA MAFUNDI 400 KUPATA VYETI VYA KUONGEZA UJUZI NA KUBORESHA BIASHARA ZAO.
By Dayo Radio
Published on 28/08/2026 20:17
News

Ni afuenisasakwa wafanyabiasharaza kiufundi humu nchini, hasa mafundi bomba, wamehimizwa kuendelea kujifunza na kuongeza ujuzi wao, kufanya kazi kwa ubora na kuwa waaminifu kwa wateja, kwa sababu sifa nzuri ni muhimu katika kazi ya ufundi

Ujumbe huo umetolewa katika kongamano lilofanyika mapema leo jijini Nairobi kwa kauli mbiu FUNDI BORA KAZI BORA Kazi, ambalo limewaleta pamoja mafundi kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kupata maarifa mapya yanayoweza kuwasaidia katika kazi zao. Kongamano hilo pia limewalenga kuwapa mafundi nafasi ya kuelewa teknolojia mpya na namna ya kutumia ujuzi wao kujenga biashara zinazoweza kuwapatia kipato cha kudumu.

Akizungumza katika kongamano hilo, mwanzilishi wa BioTank Africa, Edwin Kirugo, amesema wafundi wanapaswa kutoa huduma nzuri na kujenga uaminifu kwa wateja.

“Dumisha viwango vya juu vya kazi na uwe mwaminifu. Kama fundi, sifa yako ndiyo mtaji wako,” amesema Kirugo.

Kirugo amesema mteja anapopata huduma nzuri, salama na yenye ubora, huwa na imani zaidi na fundi na anaweza kumtambulisha kwa wateja wengine. Kwa hivyo, wafundi wamehimizwa kuzingatia ubora wa kazi zao na kutimiza ahadi wanazowapa wateja.

Jukwaa hilo pia limeangazia nafasi ya wanawake katika sekta ya ufundi, huku ikisisitizwa kuwa wanawake wanapaswa kupata ujuzi, kujenga mahusiano ya kikazi na kutumia fursa zilizopo.

Washiriki wameeleza kuwa sekta ya ufundi ina nafasi kubwa ya kutoa ajira na kuwawezesha vijana na wanawake kujitegemea. Kupitia mafunzo na mikutano kama hii, wafundi wanaweza kupata taarifa kuhusu fursa za kazi, kujifunza kutoka kwa wenzao na kuendelea kuboresha uwezo wao.

Miongoni mwa washiriki ni Nellygrace Korika, mwenye umri wa miaka 25, fundi bomba kutoka Njiru, Kasarani jijini Nairobi, mwenye uzoefu wa miaka miwili. Korika amesema amehudhuria jukwaa hilo ili kujifunza, kupata maarifa mapya na kukutana na watu wengine katika sekta hiyo.

“Kama wanawake, tunaweza pia kuwa mafundi bomba wazuri. Nimekuja hapa kujifunza na kukutana na watu wengine. Kazi ya mabomba inaendelea kubadilika, hivyo nilitaka kujua mbinu mpya. Pia matukio kama haya yanatupa nafasi za kupata kazi,” amesema Korika.

Ushiriki wa Korika umeonyesha namna wanawake wanavyozidi kuingia katika taaluma ambazo hapo awali zilionekana kutawaliwa zaidi na wanaume. Washiriki wamehimizwa kuendelea kupeana moyo na kutumia fursa za mafunzo ili kujenga taaluma zao.

Kwa upande mwingine, wafundi wenye uzoefu wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kukuza biashara zao na kuboresha huduma wanazowapa wateja.

Hassan Isadia, fundi bomba kutoka Eldoret mwenye uzoefu wa miaka 10 na ambaye ameshiriki katika kongamano hilo kwa miaka minne mfululizo, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kukuza biashara yake.

“Mafunzo haya yamenisaidia kukuza biashara yangu. Ninapata wateja zaidi kwa sababu ninapata ujuzi wa hivi karibuni. Ninafurahi pia kupata cheti kutoka NCA leo,” amesema Isadia.

Hata hivyo ameteja, kupata ujuzi mpya kumekuwa na faida zaidi ya kuboresha kazi pekee, kwa kuwa kumemsaidia pia kujenga jina katika eneo analofanyia kazi na kupata wateja wanaotambua uwezo wake. Vyeti vya kitaaluma pia vinawapa wafundi nafasi ya kuonyesha kuwa wana ujuzi unaotambulika na wanaweza kutoa huduma kwa viwango vinavyohitajika.

Wakati huohuo kongamano hilo limehusisha maonyesho ya moja kwa moja ya jinsi ya kufunga biodigester, pamoja na mafunzo kuhusu ufungaji wa 3-Chamber Biodigester, matengenezo na usalama wa kazi. Mafunzo hayo yamewapa wafundi ujuzi mpya wa kuwasaidia kuboresha huduma zao.

Mbali na mafunzo ya kiufundi, mafundi wamejifunza namna ya kukuza biashara zao, kusajili na kurasimisha shughuli zao na kupata wateja zaidi. Pia wamepata ushauri kutoka kwa wataalamu kuhusu njia bora za kufanya kazi na matumizi ya teknolojia mpya katika ujenzi na usimamizi wa maji taka.

Mafunzo hayo yamejikita pia katika matumizi ya biodigester kama njia ya kisasa ya kushughulikia maji taka. Wafundi wamepata nafasi ya kuona kwa vitendo namna mfumo wa 3-Chamber Biodigester unavyofungwa, namna ya kuutunza na hatua za kuzingatia ili kuhakikisha usalama wakati wa kazi. Ujuzi huu unaweza kuwasaidia wafundi kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wanaohitaji mifumo ya kisasa ya usimamizi wa maji taka.

Ili kutambua ujuzi wao, baadhi ya washiriki wamepatiwa vyeti kutoka National Construction Authority (NCA). Vyeti hivyo vinasaidia kuongeza uaminifu wa wafundi na kuboresha viwango vya huduma wanazotoa kwa wateja.

 

Jukwaa hilo limeandaliwa na BioTank Africa, kampuni iliyoanzishwa mwaka 2018 na Edwin Kirugo na inayotoa suluhisho za kisasa za usimamizi wa maji taka. Kampuni hiyo hutengeneza na kusambaza biodigester za plastiki na zege ambazo ni rafiki kwa mazingira na zinazoweza kutumika katika nyumba, biashara na taasisi. Bidhaa zake ni pamoja na BioTank Biodigesters, Grease Trap Pro, Bio Clean Septic Tank Enzymes na Tazo Natural Home Cleaning Products.

 

Kupitia jukwaa hili, BioTank Africa imeendelea kutoa nafasi kwa wafundi kupata maarifa yanayohusiana na bidhaa na teknolojia za kisasa katika sekta ya usimamizi wa maji taka. Lengo ni kuwasaidia mafundi kuelewa teknolojia hizo na kuzitumia kwa usahihi wanapowahudumia wateja. Kwa ujumla, Jukwaa la Fundi Bora Kazi Bora limekuwa nafasi ya kujifunza, kujenga mitandao ya kikazi, kupata vyeti na kutafuta njia mpya za kukuza biashara za wafundi.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!