Timu ya raga ya Kabras Sugar ndio mabingwa wapya wa Makala ya 36 ya SportPesa National 7s Circuit, baada ya kumfunga Bingwa mtetezi KCB kwa alama 15 kwa 5 katika fainali ya Kukata na shoka iliyochezwa mjini Mombasa, siku ya Jumapili.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ushindi huo, kocha msaidizi wa Kabras Sugar Ntabeni Dukisa amesema ushindi huo umewapa nguvu baada ya timu hiyo kusajili matokeo yasiyoridhisha katika mashindano ya Kabeberi 7s.
Dukisa amesema Kabras Sugar iliweka juhudi kubwa kurejea katika ubora na kiwango chake kabla ya fainali hiyo huku akiwapongeza wachezaji kwa kujituma na kupambana hadi kutwaa ubingwa huo.

"Tumekua na pressure kubwa sana kwa mchezo huu haswa baada ya kupata matokeo duni kababeri 7s hivyo imetulazimu kujituma sana hadi kupata ushindi huu na nafurahi sana kuona jinsi vijana walivyojituma uwanjani"
Kocha wa KCB Andrew Amonde amesema ushindi wa Kabras Sugar ni changamoto kwao kuelekea mashindano yajayo akiongeza timu hiyo itafanya maandalizi zaidi huku akitaja kutoshiriki kwa baadhi ya wachezaji katika mchezo huo kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia timu hiyo Kusuasua na hatimaye kupoteza fainali.

“Ushindi wa Kabras ni changamoto na funzo kwetu. Tutapanga mikakati upya na tutakaporejea, tutakuwa imara zaidi. Leo tumeshindwa pia kutokana na baadhi ya wachezaji wetu kutoweza kushiriki katika mashindano haya, lakini tutarekebisha mapungufu hayo kabla ya mchezo ujao"
Kutokana na ushindi huo, Kabras Sugar imetia Kibindoni elfu 150 pamoja na kujinyakulia tiketi za ndege kwa hisani ya Safarilink huku nafasi ya Pili KCB ikituzwa elfu 75 nayo Daystar Falcons RFC ikishinda elfu 40 Kwa kumaliza nafasi ya 3.
Zitech Oaks walitetea taji lao la Divisheni ya Pili Baada ya kuifunga Stallions alama 36 Kwa 7 huku wakituzwa elfu 70 Kwa ushindi huo.

Afisa wa Mahusiano ya Umma, Mauzo na Matangazo wa SportPesa Mercy Kabui, ameipongeza Kabras Sugar kwa kutwaa ubingwa na kuwataka wachezaji chipukizi wenye shauku na vipaji katika mchezo wa raga kujitokeza na kuonyesha uwezo wao.

Kabui amesema SportPesa itaendelea kuunga mkono mashindano hayo kama jukwaa la kukuza vipaji na kuwapa wachezaji nafasi ya kufikia viwango vya juu katika mchezo wa raga.
“Ni fursa nzuri ya kuonyesha kipaji chako, kwa sababu hujui kitakachotokea au nani anaweza kukugundua. Kwa mtu ambaye amemaliza shule ya upili na anaamini ana uwezo wa kucheza raga, anaweza kuanzia mahali fulani na SportPesa 7s Circuit ni jukwaa sahihi la kuonyesha kipaji chake.”
Mabingwa wapya Kabras Sugar walifuzu kwa fainali hiyo baada ya kuifunga Daystar Falcons alama 19 Kwa 5 huku KCB ikitinga fainalini Kwa kuilabua Menengai Oilers alama 10 Kwa 5.
Daystar Falcons wamemaliza mashindano hayo Katika nafasi ya 3 Baada ya Kuwachabanga Menengai Oilers alama 21-5 .
Baada ya kukamilika kwa Makala ya 36 ya Driftwood 7s, mashindano yajayo katika SportPesa National 7s Circuit yatakuwa Embu 7s, huku timu zikitarajiwa kuendeleza ushindani wa kuwania ubingwa wa msimu huu.