Zawadi nono zachochea ushindani SportPesa National 7s Circuit
By Dayo Radio
Published on 23/08/2026 06:58
News

Ushindani umezidi kupamba moto katika makala ya 36 la mashindano ya Driftwoods 7s ya mchezo wa raga, huku waandaaji wakiongeza kitita cha zawadi kwa washindi .

Akizungumza na wanahabari, Afisa wa mahusiano ya umma, Mauzo na Matangazo Kampuni ya Sportpesa Mercy Kabui , amesema mfumo mpya wa zawadi umewekwa katika mashindano ya mwaka huu ili kuwapa wachezaji motisha zaidi na kuongeza ushindani uwanjani 

Kabui amesema uwekezaji katika zawadi ni sehemu ya juhudi za kuibua na kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo.

"Mwaka huu tumeongeza mara mbili kiwango cha zawadi kwa washindi ikilinganishwa na mwaka uliopita, kwa sababu mchezo huu una ushindani mkubwa. Tunataka pia kuhamasisha timu zaidi kushiriki katika michezo na kama SportPesa tunapenda sana kuwaunga mkono vijana katika michezo mbalimbali si raga pekee.”

Hata hivyo kabui amesema kuwa ushiriki wa wanawake katika raga hasa mjini Mombasa bado ni kidogo huku akizitaka timu na wachezaji wanawake kujitokeza kwa wingi katika mashindano yajayo.

“Tumekuwa na changamoto ya wanawake kushiriki katika michezo, hasa hapa Mombasa. Tunawataka wanawake kujitokeza na kushiriki katika mashindano haya mwakani, kwa sababu hadi sasa Mombasa ndiyo kaunti pekee ambayo haina timu ya wanawake.”

Wakati huo huo kabui amebainisha kuwa SportPesa imeweka mipango wa kuleta ushiriki wa watu wenye ulemavu katika michezo kuanzia mwaka ujao .

“Tunatumaini kwamba mwakani tutaweza kufungua nafasi kwa watu wenye ulemavu ili nao washiriki katika michezo. Hata kama si raga, tunaamini wanaweza kushiriki katika michezo mingine na kuonyesha vipaji vyao.”

Fauka ya hayo ni kwamba baadhi ya timu zimerekodi ushindi wa kuvutia katika michezo ya jumamosi ambapo Stallions Rugby 7s iliichapa KCNP 7s kwa alama 43 kwa nunge, huku CUEA Monks 7s ikiibuka na ushindi mkubwa wa alama 47 kwa 7 dhidi ya South Coast Pirates 7s.

JKUAT Cougars 7s nayo ilipata ushindi wa alama 29 kwa 5 dhidi ya Malindi Turtles, huku Embu 7s ikiifunga Shanzu Marlins 7s kwa alama 31 kwa nunge, Mean Machine 7s iliifunga MKU Thika 7s kwa 24 kwa nunge huku Impala 7s ikiichapa Jackals 7s kwa alama 19 kwa 5.

Ikumbukwe kuwa Mashindano ya Driftwoods 7 yanaendelea huku kilele cha mashindano hayo kikitarajiwa Jumapili.

Comments
Comment sent successfully!