VIONGOZI WA KIDINI WAUNGA MKONO AGIZO LA WAZIRI WA ELIMU KUHUSU MUDA WA MASOMO.
By Dayo Radio
Published on 20/08/2026 14:43
News

Kufatia agizo la waziri wa elimu, Julius Ogamba la kuzitaka shule zote za umma na binafsi kuzingatia kikamilifu muda rasmi wa masomo kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tisa na nusu alasiri, viongozi wa kidini ukunda wa pwani wakiongozwa na Sheikh Abu Qatada, wamesema utekelezaji wake utawapa wazazi nafasi zaidi ya kuwa na watoto wao baada ya masomo na kushiriki kikamilifu katika malezi yao.Akizungumza na wanahabari mapema leo  Sheikh Abu Qatada amesema, hatua hii itasaidia pakubwa kuwapa wazazi nafasi ya kukaa na watoto wao baada ya masomo, kuwafuatilia kwa karibu na kuwafunza maadili mema.

Sheikh Abu Qatada ameongeza kuwa muda huo utasaidia pia kujenga mahusiano mazuri ya kifamilia, akisema wazazi watapata nafasi ya kuwafundisha watoto wao nidhamu, uwajibikaji na maadili mema.

Aidha, Sheikh Abu Qatada amesema hatua hiyo imetoa fursa nzuri kwa watoto kupata mafunzo ya kidini nje ya muda wa masomo, akisisitiza kuwa elimu hiyo ina nafasi muhimu katika kuwajenga watoto kimaadili.

“Tumepata fursa nzuri ya kuwafunza watoto wetu masomo ya kidini pamoja na maadili yanayohitajika katika maisha yao. Ni muhimu mtoto kupata elimu ya darasani lakini pia akalelewe katika misingi mizuri ya maadili,” amesema Sheikh Abu Qatada.

Viongozi hao wametoa wito kwa shule zote za umma na binafsi kuzingatia kikamilifu muda uliowekwa na Wizara ya Elimu, wakisema hatua hiyo itasaidia kuweka uwiano kati ya masomo ya darasani, malezi ya familia na mafunzo ya kidini.

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!