Serikali imeendelea na utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa usajili na utambuzi wa mifugo kupitia mfumo wa Animal Identification and Traceability (ANITRAC), huku waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Mutahi Kagwe, akiongoza zoezi la uhamasishaji na uwekaji wa alama za utambuzi kwa mifugo katika eneo la Kurawa, Kaunti ya Tana River.
Katika ziara hiyo, waziri Kagwe ameandamana na Seneta wa Tana River, Danson Mungatana, pamoja na maafisa kutoka Idara ya huduma za mifugo (DVS), ambapo wamekutana na wafugaji na viongozi wa eneo hilo ili kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa mfumo wa ANITRAC.

Akizungumza na wafugaji, waziri Kagwe amesema mfumo huo ni hatua muhimu katika kuifanya sekta ya mifugo kuwa ya kisasa na yenye ushindani wa kimataifa.
"ANITRAC si zoezi la kuweka alama kwenye mifugo pekee. Ni msingi wa uchumi wa kisasa wa mifugo ambapo kila mnyama aliyesajiliwa anapata utambulisho wa kidijitali unaowezesha kufuatilia historia yake kuanzia alikotoka hadi anapofikishwa sokoni," amesema Waziri Kagwe.
Ameeleza kuwa masoko ya kimataifa yanahitaji bidhaa za mifugo zinazoweza kufuatiliwa kwa urahisi, huku wanunuzi wakitaka kujiridhisha kuhusu mahali mnyama alikotoka, historia ya usafirishaji wake na hali yake ya afya kabla ya kuruhusu bidhaa hizo kuingia katika masoko yenye thamani kubwa.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la usajili wa mifugo.
"Serikali imejipanga kufungua masoko yenye thamani kubwa barani Ulaya, mashariki ya kati na maeneo mengine duniani. Hata hivyo, mafanikio yatategemea ushiriki wa wafugaji katika mfumo wa utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo unaokidhi viwango vya kimataifa," amesema.

Aidha amebainisha kuwa Kenya ina takribani mifugo milioni 77, huku sekta hiyo ikichangia asilimia 12 ya pato la Taifa (GDP) na asilimia 40 ya pato la sekta ya kilimo.
Hata hivyo amesema mfumo wa ANITRAC utaimarisha udhibiti wa magonjwa ya mifugo, kupunguza wizi wa mifugo, kuboresha usalama wa chakula na kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo katika masoko ya ndani na nje ya nchihuku alama za utambuzi na vifaa vya kielektroniki vinavyotumika katika mfumo huo vinazalishwa nchini, hatua ambayo inasaidia kukuza viwanda vya ndani na kutoa ajira kwa Wakenya.
Katika upande wa uwekezaji uwekezaji wa Serikali katika Viwanda vya Ngozi vya Kenya (Kenya Leather Industrial Parks), ametaja hatua hiyo kuwa itasaidia nchi kuuza bidhaa za ngozi zilizoongezwa thamani badala ya ngozi ghafi.
"Maono ya Serikali ni kuibadilisha sekta ya mifugo kutoka mfumo wa kujikimu na kuwa biashara ya kisasa inayozalisha utajiri, kuendeleza viwanda na kuiwezesha Kenya kuwa miongoni mwa wasambazaji wanaoaminika wa bidhaa salama, zenye ubora na zinazoweza kufuatiliwa katika soko la kimataifa," amesema Waziri Kagwe.
Serikali imesema utekelezaji wa mfumo wa ANITRAC utaendelea katika kaunti zote nchini huku usajili wa mifugo ukipewa kipaumbele ili kuongeza mapato ya wafugaji, kupanua masoko ya bidhaa za mifugo na kuimarisha sekta hiyo nchini.
NA HARRISON KAZUNGU.