Waziri wa usalama wa ndani na utawala wa kitaifa, Kipchumba Murkomen, ametoa onyo kali kwa watu wanaodaiwa kufadhili, kupanga na kuwezesha mashambulizi ya ujambazi katika kaunti za Samburu, West Pokot, Tiaty na Isiolo, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kukabiliana kikamilifu na mtandao wa wahalifu hao na kuwafikisha wote wanaohusika mbele ya sheria.
Akizungumza katika eneo la Lolmolok, wadi ya Suguta, Kaunti ya Samburu, wakati wa ziara yake ya kutathmini hali ya usalama na utoaji huduma za Serikali, Murkomen amesema vyombo vya usalama vina taarifa za kutosha za kuhusu watu wanaofadhili, kuratibu na kuwezesha mashambulizi ya majambazi katika maeneo hayo, na kwamba hakuna atakayesalimika wakati operesheni hiyo itakapoanza.
"Tunawajua mlipo, na tutawafuata. Kupitia operesheni za kiintelijensia, tutawapata popote mlipo bila kujali nyinyi ni kina nani, na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yenu," amesema Murkomen.

Waziri huyo amesema Serikali haitapambana na wahalifu wanaotekeleza mashambulizi pekee, bali pia itawakabili watu wote wanaowapa fedha, silaha, taarifa na msaada wa aina yoyote unaowezesha uhalifu huo kuendelea. Amesema mtandao mzima wa uhalifu huo utavunjwa ili kurejesha amani katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Murkomen ametangaza kuwa Serikali imeidhinisha kuanza kwa operesheni kubwa ya pamoja ya usalama itakayoongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, akieleza kuwa operesheni hiyo itahusisha vikosi mbalimbali vya usalama vitakavyofanya msako mkali dhidi ya majambazi na washirika wao.
Waziri huyo amewataka wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa hiari kwa vyombo vya usalama kabla ya operesheni hiyo kuanza rasmi, akionya kuwa watakaokaidi agizo hilo watakabiliwa na hatua kali za kisheria.
Amesema lengo kuu la operesheni hiyo ni kurejesha hali ya usalama katika maeneo yaliyokumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara, kuhakikisha wananchi waliokimbia makazi yao wanarejea nyumbani kwa usalama, pamoja na kuruhusu shughuli za kiuchumi, elimu na huduma nyingine za kijamii kurejea katika hali ya kawaida.

"Tulivyofanikiwa kurejesha amani katika maeneo mengine ya Bonde la Kerio, ndivyo tutakavyofanya hapa hadi eneo hili litakapokuwa salama kabisa. Serikali haitachoka hadi wananchi waweze kuishi bila hofu," amesisitiza Murkomen.
Mbali na operesheni hiyo, Murkomen ametangaza hatua nyingine za muda mrefu za kuimarisha usalama katika eneo hilo. Amesema Serikali itaongeza idadi ya Maafisa wa Akiba wa Polisi wa Kitaifa (National Police Reservists), kujenga vituo vipya vya usalama, kuboresha mtandao wa barabara ili kurahisisha doria za maafisa wa usalama, pamoja na kupanua huduma za mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo bado hayana mtandao wa kutosha.
Hata hivyo ameongeza kuwa serikali inaamini kuwa kuboresha miundombinu na huduma za msingi kutasaidia kuongeza kasi ya maendeleo na kupunguza changamoto zinazochochea uhalifu katika maeneo ya wafugaji.
Murkomen pia ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, wazee wa jamii, viongozi wa dini na wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahalifu na kuvunja mitandao yao.

Katika ziara hiyo, Murkomen ameandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Utawala (APS) Gilbert Masengeli, Kamanda wa Kikosi cha GSU Johana Tonui pamoja na maafisa wengine wakuu wa Serikali.
Viongozi, waluonganaungana katika hafla hiyo ni pamoja na gavana wa Samburu Jonathan Lelelit, Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda, Mbunge wa Samburu Kaskazini Eli Letipila, aliyekuwa Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal, pamoja na Waheshimiwa Mawakilishi wa Wadi wakiongozwa na MCA wa Wadi ya Suguta James Leleruk, ambao wameeleza dhamira yao ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha amani na usalama vinarejea katika maeneo yote yaliyoathiriwa na ujambazi.
NA HARRISON KAZUNGU.