VIONGOZI WA KIDINI WAKEMEA TAMASHA LA SUMMERTIDE, WATAKA SERIKALI KULIPIGA MARUFUKU
By Dayo Radio
Published on 09/07/2026 15:50
News

Viongozi wa kidini jijini Mombasa kupitia muungano wa Pwani Patriotic Religious Leaders (PPRL) wamekemea vikali tamasha la Summertide lililofanyika mjini Malindi, wakisema kuwa limekiuka maadili ya kidini, tamaduni na mila za Kiafrika. Viongozi hao wameonya kuwa matamasha ya aina hiyo yanachangia mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana na kuhatarisha mustakabali wa kizazi kijacho.

Wakizungumza na wanahabari mapema leo wakiongozwa na Sheikh Abu Qatada, viongozi hao wamesema baadhi ya washiriki wa tamasha hilo walivaa mavazi yasiyofaa na kufanya vitendo ambavyo havikubaliki katika jamii. Wameitaka serikali kuingilia kati kwa kuweka masharti makali kwa waandaaji wa matamasha ya burudani na, pale inapobidi, kuyapiga marufuku ili kulinda maadili ya jamii.

"Tunachokiona katika matamasha ya aina hii si burudani tena, bali ni vitendo vinavyovunja maadili na kuheshimiana katika jamii. Hatuwezi kukaa kimya huku vijana wetu wakivutwa kwenye maisha yasiyo na mwelekeo. Tunaitaka serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha matamasha yanayokiuka maadili, tamaduni na mila za Kiafrika hayapati nafasi ya kufanyika nchini," amesema Sheikh Abu Qatada.

Ameongeza kuwa waandaaji wa matamasha hayo wanaonekana kuweka mbele maslahi ya kifedha kuliko ustawi wa jamii, akisema kuwa faida wanazopata haziwezi kulinganishwa na athari zinazowaandama vijana na familia zao.

"Faida ya watu wachache haiwezi kuwa muhimu kuliko mustakabali wa taifa. Tunahitaji mazingira yatakayowalea vijana katika misingi ya heshima, nidhamu na maadili mema badala ya kuwapa jukwaa la kuharibu maisha yao," ameongeza.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Askofu Paul Mwaura, ambaye amesema matamasha kama hayo yamekuwa yakitumiwa kama mianya ya ulanguzi wa mihadarati, matumizi mabaya ya vileo na kuchochea vitendo vya ngono miongoni mwa vijana. Amesema hali hiyo inahatarisha afya, usalama na maendeleo ya kizazi kijacho.

"Serikali inapaswa kuwawajibisha waandaaji na wafadhili wa matamasha haya kwa kuhakikisha sheria zinafuatwa kikamilifu. Hatuwezi kuruhusu matukio yanayoweka watoto na vijana wetu katika mazingira yanayochochea matumizi ya mihadarati, ulevi na tabia nyingine zinazoharibu maisha yao," amesema Askofu Mwaura.

Amesisitiza kuwa viongozi wa kidini wataendelea kushirikiana na serikali, wazazi na wadau wengine katika kuhamasisha jamii kulinda maadili na kuhakikisha burudani inayotolewa nchini inazingatia utu, heshima na maadili yanayokubalika katika jamii.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!