Shirika la maendeleo la Uswisi, Swisscontact, linalojihusisha na kukuza ujuzi wa kazi, maendeleo ya sekta binafsi na ajira kwa vijana katika mataifa mbalimbali, limezindua rasmi mpango wa PropelA katika Kaunti ya Mombasa kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika na waajiri pamoja na kuongeza nafasi za ajira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Programu wa Swisscontact, Jimmy Delyon, amesema mpango wa PropelA umeonyesha mafanikio makubwa katika maeneo uliotekelezwa awali, ambapo kampuni zilizoshiriki zimeripoti kuongezeka kwa tija pamoja na kurejesha hadi asilimia 30 ya gharama walizowekeza katika mafunzo ya wanafunzi waliokuwa wakijifunza kwa vitendo.

Delyon amesema mafanikio hayo yameipa Swisscontact sababu ya kupanua utekelezaji wa mpango huo hadi Mombasa ili kuwafikia vijana wengi zaidi katika Ukanda wa Pwani na kuwapa fursa ya kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta zinazokua kwa kasi.
Pia amefafanua kuwa PropelA inalenga kuziba pengo lililopo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo ya vitendo kupitia ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za mafunzo na waajiri.
Aidha, amewahimiza waajiri kushirikiana kwa karibu na vyuo vya ufundi na taasisi za mafunzo kwa kufungua nafasi zaidi za mafunzo kazini ili kuwapa vijana uzoefu unaohitajika kabla ya kuingia rasmi katika soko la ajira.

"Hatutaki kuona vijana wakibaki na vyeti bila kazi. Tunataka waondoke vyuoni wakiwa na maarifa, ujuzi na uzoefu unaowafanya waajiri wawahitaji mara moja. Hii ndiyo dira ya PropelA na mchango wetu katika kujenga nguvu kazi yenye ushindani nchini Kenya," amesema Delyon.
Mpango wa PropelA unatekelezwa na Swisscontact kwa ushirikiano na sekta binafsi, Mamlaka ya Taifa ya Mafunzo ya Viwandani (NITA) pamoja na taasisi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), ukiwa na lengo la kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi, kuongeza ajira kwa vijana na kuhakikisha sekta ya viwanda nchini inapata wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.