Benki ya Absa Kenya kwa ushirikiano na kampuni ya Unilever Kenya wamezindua mpango wa ufadhili wenye thamani ya Shilingi bilioni 4, unaolenga kuongeza upatikanaji wa mtaji kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), hatua inayotarajiwa kuimarisha usambazaji wa bidhaa na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi nchini.
Mpango huo unalenga zaidi ya wasambazaji 38 wa Unilever Kenya pamoja na wauzaji na wahifadhi wa bidhaa katika msururu wake wa usambazaji.

Katika awamu ya kwanza, zaidi ya wasambazaji 10 wanatarajiwa kujiunga na mpango huo kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Kupitia huduma ya Wezesha Stock Loan, wafanyabiashara watapata suluhisho la haraka, rahisi na la kuaminika la kupata mtaji wa biashara, hatua itakayowasaidia kuongeza kiwango cha bidhaa sokoni, kupanua shughuli zao na kuboresha huduma kwa wateja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Absa Bank Kenya, Yusuf Omari, amesema benki hiyo imeendelea kushirikiana na wafanyabiashara katika sekta ya usambazaji wa bidhaa kwa miongo kadhaa huku ushirikiano mpya na Unilever ukilenga kupanua fursa za ukuaji kwa wasambazaji na wauzaji.

"Kwa miongo kadhaa, Absa imekuwa mshirika wa wafanyabiashara katika mfumo wa usambazaji wa bidhaa nchini. Ushirikiano huu na Unilever unapanua fursa kwa wasambazaji na wauzaji kupata mtaji kwa wakati, hivyo kuwawezesha kukuza biashara zao na kuimarisha msururu mzima wa usambazaji," amesema Omari.
Hata hivyo ameongeza kuwa kupitia mfumo wa kidijitali wa Wezesha Stock, wafanyabiashara wataweza kupata mikopo isiyo na dhamana ya hadi Shilingi milioni 10, ikiwemo ufadhili wa LPO, ankara na mali hadi Shilingi milioni 5 zikitolewa ndani ya saa 48 kupitia mfumo huo wa kidijitali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Unilever Kenya, Luck Ochieng, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu ya kuimarisha mnyororo wa usambazaji wa kampuni hiyo huku ukiwawezesha wasambazaji wake kukua kwa njia endelevu.

"Wasambazaji wetu wanaohudumia zaidi ya wauzaji 140,000 nchini ndio msingi wa biashara yetu. Ushirikiano huu na Absa unawapa fursa ya kupata ufadhili wa haraka na wenye unafuu, jambo litakalowawezesha kukuza biashara zao, kuboresha upatikanaji wa bidhaa na kuwahudumia vyema zaidi wateja," amesema Ochieng.
Mpango huo unatarajiwa kuimarisha biashara ndogo na za kati ambazo ni mhimili wa sekta ya bidhaa za matumizi nchini, kuongeza ajira, kukuza uthabiti wa biashara na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Aidha, unaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Absa Bank Kenya na Unilever ulioanza mwaka 1980, ukiwa na lengo la kuimarisha maendeleo endelevu na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa thamani nchini.
NA HARRISON KAZUNGU