MELI YA KIFAHARI YENYE WATALII ZAIDI YA 1,000 YATIA NANGA MOMBASA, YAONGEZA MATUMAINI YA KUKUA KWA SEKTA YA UTALII NCHINI
By Dayo Radio
Published on 30/06/2026 15:04
News

Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) imepokea rasmi meli ya kwanza ya watalii kutoka bara la Asia iliyowasili katika Bandari ya Mombasa ikiwa imebeba zaidi ya watalii 1,000 wanaotarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini kabla ya kuendelea na safari yao kuelekea mataifa mengine.

Ujio wa meli hiyo unatajwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha utalii wa baharini nchini, huku ukionyesha kuendelea kurejea kwa shughuli za utalii baada ya kuongezeka kwa idadi ya meli za kitalii zinazotia nanga katika Bandari ya Mombasa.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya wageni hao, Mkurugenzi Mkuu wa KPA amesema mamlaka hiyo imeendelea kuboresha miundombinu na huduma bandarini ili kuhakikisha wageni wanaowasili nchini wanapata huduma bora na uzoefu mzuri tangu wanapowasili.

 

Amesema kuwasili kwa watalii hao kutakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa, hasa kwa sekta za utalii, usafirishaji, biashara na huduma za hoteli, kwani wageni hao watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kutumia huduma zinazotolewa na wafanyabiashara wa ndani.

"Tunafurahia kuipokea meli hii pamoja na wageni wake zaidi ya 1,000. Hii ni ishara kuwa Kenya inaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha utalii wa baharini katika ukanda wa Afrika Mashariki. Wageni hawa watatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kupitia matumizi yao katika sekta mbalimbali za utalii na biashara," amesema.

Aidha, amesema Mamlaka ya Bandari Kenya ina matarajio ya kupokea jumla ya meli 20 za watalii kufikia mwisho wa mwaka huu, jambo ambalo linaashiria kuongezeka kwa imani ya kampuni za kimataifa za usafiri wa baharini kuendelea kuijumuisha Kenya katika ratiba zao za safari za kitalii.

Kwa upande wake, nahodha wa meli hiyo, Alex Sehlstedt, ameipongeza Kenya kwa maandalizi mazuri na mapokezi ya wageni hao, akisema hali ya usalama, huduma bora na ukarimu wa Wakenya ni miongoni mwa sababu zinazowavutia watalii wengi kutembelea nchi hiyo.

"Tunashukuru kwa mapokezi mazuri tuliyoyapata tangu tulipowasili Bandari ya Mombasa. Ushirikiano huu unaendelea kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na sekta ya kimataifa ya utalii wa baharini. Tunaamini wageni wetu watakuwa na uzoefu mzuri wakati wa ziara yao nchini," amesema.

Nahodha huyo ameongeza kuwa meli hiyo imebeba wageni kutoka mataifa 16, ambao watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini ikiwemo mbuga za wanyama, maeneo ya kihistoria na fukwe za Pwani kabla ya kuendelea na safari yao kupitia mataifa mengine na kuhitimisha ziara yao nchini Uhispania.

Wadau wa sekta ya utalii wameeleza matumaini kuwa kuongezeka kwa idadi ya meli za watalii zinazowasili nchini kutasaidia kuongeza mapato ya taifa, kuimarisha biashara za wenyeji, kuzalisha ajira na kuendeleza ukuaji wa sekta ya utalii ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Kenya.

 

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online