Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) imetangaza rasmi kuwa uchaguzi mkuu ujao nchini Kenya utafanyika tarehe 10 Agosti 2027 huku ikizindua ratiba ya shughuli muhimu zitakazoongoza maandalizi na utekelezaji wa mchakato mzima wa uchaguzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ratiba hiyo, kamishna wa IEBC, Ann Nderitu, amesema kuwa tume imeweka tarehe mahsusi za shughuli mbalimbali ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa njia ya uwazi, haki na kwa mujibu wa katiba pamoja na sheria za uchaguzi nchini.
Nderitu amesema kuwa maafisa wote wa umma wanaonuia kuwania nyadhifa za kisiasa katika uchaguzi huo watahitajika kujiuzulu kutoka nyadhifa zao kufikia tarehe 9 Februari 2027.
"Maafisa wote wa umma wanaotarajia kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wanapaswa kujiuzulu kufikia tarehe 9 Februari 2027 kwa mujibu wa matakwa ya Katiba na sheria za uchaguzi," amesema Nderitu.
Amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha usawa katika ushindani wa kisiasa na kuondoa uwezekano wa matumizi mabaya ya ofisi za umma wakati wa kampeni za uchaguzi.

Wakati huohuo, vyama vya kisiasa vimetakiwa kuwasilisha sajili za wanachama wao pamoja na ratiba za uteuzi wa wagombea kufikia tarehe 16 Machi 2027 ili kuwezesha tume kufanya uhakiki wa taarifa hizo mapema kabla ya kuanza kwa shughuli nyingine za uchaguzi.
"Vyama vya kisiasa vitahitajika kuwasilisha sajili zao za wanachama na ratiba za uteuzi wa wagombea kufikia tarehe 16 Machi 2027 ili kuwezesha tume kusimamia mchakato huo kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria," ameongeza.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, vyama vya kisiasa vitapaswa kukamilisha michakato yao ya mchujo wa wagombea pamoja na kutatua migogoro yote ya uteuzi ifikapo tarehe 9 Mei 2027.
Nderitu amesema kuwa kukamilika kwa mchakato huo kwa wakati kutasaidia kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa uteuzi rasmi wa wagombea.
"Vyama vya kisiasa vinapaswa kuhakikisha kuwa mchujo wa wagombea na utatuzi wa migogoro yote inayohusiana na uteuzi unakamilika kufikia tarehe 9 Mei 2027," amesema.
Aidha, watu wanaonuia kuwania nyadhifa za uchaguzi kama wagombea huru wametakiwa kujiondoa rasmi katika vyama vya kisiasa kabla ya tarehe hiyo ili kutimiza masharti ya kisheria yanayowawezesha kushiriki katika uchaguzi kama wagombea huru.
Kamishna huyo amesema kuwa uteuzi rasmi wa wagombea utafanyika kati ya tarehe 29 Mei na 11 Juni 2027 ambapo wagombea wote watatakiwa kuwasilisha nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya kuthibitishwa na tume.
"Zoezi la uteuzi wa wagombea litafanyika kuanzia tarehe 29 Mei hadi 11 Juni 2027 ambapo wagombea wote watatakiwa kukidhi masharti yaliyowekwa na sheria za uchaguzi," amesema.
Baada ya kukamilika kwa uteuzi huo, wagombea wataruhusiwa kuendelea na kampeni zao katika kipindi kitakachotambuliwa rasmi na tume kabla ya kampeni hizo kufungwa tarehe 7 Agosti 2027, siku tatu kabla ya wananchi kuelekea katika vituo vya kupigia kura.
"Kampeni rasmi za uchaguzi zitahitimishwa tarehe 7 Agosti 2027 ili kutoa nafasi ya maandalizi ya mwisho kabla ya siku ya uchaguzi tarehe 10 Agosti 2027," amesema Nderitu.
IEBC imesisitiza kuwa ratiba hiyo ni mwongozo muhimu kwa vyama vya kisiasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi, huku ikitoa wito kwa wote kuzingatia tarehe zilizowekwa ili kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 yanafanyika kwa utaratibu unaostahili na unaozingatia sheria za nchi. Tume hiyo pia imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
NA HARRISON KAZUNGU.