MADAI YA WATU KUPOTEZA SEHEMU ZA SIRI MOMBASA NI UVUMI WA UONGO, ASEMA KAMISHINA WA KAUNTI MOHAMMED NOOR.
By Dayo Radio
Published on 23/06/2026 13:05
News

Kamishna wa kaunti ya Mombasa Mohammed Noor amepuuzilia mbali madai yanayoendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo kuhusu watu kupoteza sehemu zao za siri, akisema kuwa madai hayo hayana msingi wowote na kwamba ni mbinu mpya inayotumiwa na wahalifu kueneza hofu miongoni mwa wananchi ili kupata mwanya wa kutekeleza vitendo vya uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mombasa, Noor amesema kuwa hadi sasa vyombo vya usalama havijapokea ushahidi wowote unaothibitisha madai hayo, akisisitiza kuwa taarifa hizo ni porojo zinazolenga kuwapotosha wananchi na kuzua taharuki isiyo ya lazima.

"Madai haya ni porojo tu na hayana msingi wowote. Kufikia sasa hatujapata ushahidi wowote unaothibitisha kwamba kuna mtu amepoteza sehemu zake za siri. Hii ni mbinu mpya inayotumiwa na wahalifu kueneza hofu na kuwahadaa wananchi ili wapate nafasi ya kuwaibia au kufanya vitendo vingine vya uhalifu," amesema Noor.

Kamishna huyo amesema kuwa serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa zinazotolewa na wananchi na kuhakikisha kuwa usalama wao unadumishwa wakati wote, huku akiwataka wakazi wa Mombasa kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida.

Vilevile, Noor ametoa onyo kali kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaoendelea kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, akisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana akieneza habari za uongo ambazo zinaweza kuhatarisha usalama na mshikamano wa jamii.

"Tunawatahadharisha wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza habari za uongo kwamba sheria itawafikia. Uhuru wa kujieleza haupaswi kutumiwa vibaya kwa kusambaza taarifa za kupotosha umma. Tayari baadhi ya watu wanaohusishwa na kusambaza madai hayo wamekamatwa na uchunguzi zaidi unaendelea," ameongeza Noor.

Aidha, amesema kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kutumia uvumi huo kuwatapeli au kuwaibia wananchi, akieleza kuwa vyombo vya dola vimeimarisha doria na uchunguzi ili kuhakikisha usalama wa wakazi wa kaunti hiyo unaendelea kuimarika.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Mombasa Stella Cherono ambaye amewataka wananchi kuepuka kuchukua sheria mikononi mwao kutokana na taarifa zinazozagaa, akisisitiza kuwa njia sahihi ni kuripoti visa vyovyote vya kutatanisha kwa maafisa wa polisi ili vifanyiwe uchunguzi wa kina.

"Tunawasihi wananchi kutotwaa sheria mikononi mwao kwa msingi wa uvumi au taarifa ambazo hazijathibitishwa. Ikiwa kuna tukio lolote linalotia shaka, ni vyema liripotiwe kwa maafisa wa polisi ili hatua zinazofaa zichukuliwe. Kuchukua sheria mikononi mwao kunaweza kusababisha madhara kwa watu wasio na hatia," amesema Cherono.

Kamanda huyo ameongeza kuwa maafisa wa usalama wako macho na wanaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kushuhudiwa katika Kaunti ya Mombasa.

Kauli za viongozi hao wawili zinajiri wakati ambapo madai kuhusu watu kupoteza sehemu zao za siri yameendelea kuenea katika baadhi ya maeneo ya Mombasa na kusababisha hofu na taharuki miongoni mwa wakazi. Hata hivyo, maafisa wa usalama wamewahakikishia wananchi kuwa hakuna tukio lolote lililothibitishwa kufikia sasa, huku wakisisitiza umuhimu wa kutegemea taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka husika na kuepuka kusambaza uvumi unaoweza kuhatarisha usalama na mshikamano wa jamii.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!

Chat Online