Mkereketwa wa masuala ya uongozi na maendeleo ya jamii, Nasoro Ngao, amewahimiza vijana pamoja na wakazi wa kaunti ya Mombasa kujiunga katika vikundi mbalimbali ili waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotolewa na serikali pamoja na mashirika mbalimbali, akisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira na kupunguza kiwango cha umaskini katika jamii.
Ngao ametoa kauli hiyo wakati wa shughuli ya kusafisha taka katika ufuo wa bahari ya Wangwani uliopo eneo la Junda, katika eneobunge la Kisauni, ambapo amesema kuwa vijana wanapaswa kujipanga katika vikundi ili kuwawezesha kupata mafunzo mbalimbali, mikopo pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo inayolenga kuwainua kiuchumi na kuwapa uwezo wa kujitegemea.
Amesema kuwa kutokana na nafasi za ajira rasmi kuendelea kuwa chache nchini, ni muhimu kwa vijana kuacha kutegemea ajira za kuajiriwa pekee na badala yake kutumia fursa zinazopatikana kupitia vikundi vya kijamii na kiuchumi ili kubuni nafasi za kujiajiri na kuboresha maisha yao.

"Vijana wanapaswa kujiunga katika vikundi ili kunufaika na miradi mbalimbali inayotolewa na serikali na mashirika tofauti. Kupitia vikundi hivyo wanaweza kupata ujuzi, kujengewa uwezo, kupata mitaji na hatimaye kujikwamua kiuchumi huku wakichangia maendeleo ya jamii inayowazunguka," amesema Ngao.
Ameeleza kuwa changamoto ya ukosefu wa ajira inayowakabili vijana inaweza kupunguzwa iwapo kutakuwa na ushirikiano na kujituma katika shughuli za maendeleo, akiongeza kuwa umoja miongoni mwa vijana ni silaha muhimu katika kupambana na umaskini na kuongeza kipato katika familia nyingi.
Aidha, Ngao amesisitiza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira akibainisha kuwa taka zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kupitia shughuli za ukusanyaji, upangaji na urejelezaji wa taka, huku akiwahimiza wananchi kuunga mkono miradi inayolenga kubadilisha taka kuwa mali.
Amesema kuwa mazingira safi yanachangia afya bora kwa jamii na pia yanaweza kutoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana kupitia shughuli mbalimbali za utunzaji na usimamizi wa mazingira.

"Ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanatunzwa. Tunapaswa kuona taka kama rasilimali inayoweza kutuletea kipato na kuboresha maisha yetu. Kupitia ubunifu na ushirikiano, vijana wengi wanaweza kujiajiri na kuondokana na utegemezi," amesema.
Wakati huohuo, mkereketwa huyo wa masuala ya uongozi amewataka viongozi mbalimbali nchini kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuelekeza nguvu zao katika kuwahudumia wananchi waliowapa dhamana ya uongozi.
Amesema kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kwani wananchi wanatarajia kuona viongozi wakifanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya maslahi ya jamii badala ya kujihusisha na migogoro ya kisiasa isiyo na manufaa kwa wananchi wa kawaida.
"Ni wakati wa viongozi kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa na kushughulikia masuala yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Wananchi waliwaamini na kuwapa mamlaka ili wawahudumie, hivyo maendeleo na ustawi wa wananchi vinapaswa kuwa kipaumbele kuliko siasa za migawanyiko," amesema Ngao.
Aidha, amesema kuwa viongozi wanapaswa kuonyesha mfano bora wa mshikamano na uwajibikaji ili kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za uongozi na kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya viongozi, mashirika ya kijamii, sekta binafsi na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha jamii zinapata fursa za mafunzo, mitaji na masoko ya bidhaa na huduma mbalimbali, hali ambayo itasaidia kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Ngao pia amebainisha kuwa milango yake iko wazi kwa yeyote anayehitaji ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii, akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Shughuli hiyo ya usafi wa mazingira katika ufuo wa Wangwani imewaleta pamoja vijana, wakazi na wadau mbalimbali ambao walishiriki katika ukusanyaji wa taka huku wakipewa elimu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutumia taka kama mali inayoweza kuleta manufaa ya kiuchumi.
Washiriki wa hafla hiyo wameeleza matumaini yao kuwa kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali na kuongezeka kwa uhamasishaji wa wananchi, jamii itaendelea kunufaika na miradi ya maendeleo itakayochangia kupunguza umaskini, kuongeza ajira kwa vijana na kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo na taifa kwa ujumla.
NA HARRISON KAZUNGU.